Habari

Uchunguzi wa DNA wabainisha Sharon na Melon ni pacha

June 15th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

UCHUNGUZI wa DNA umetanzua kitendawili cha wasichana wawili kutoka Kakamega wanaofanana kama shingili kwa ya pili kwa kubaini kuwa ni pacha.

Ripoti ya DNA pia ilithibitisha kuwa Sharon Mitekwa na Melon Lutenyo kutoka Kaunti ya Kakamega walizaliwa na mama mmoja.

Kulingana na ripoti ya maabara ya Lancet Kenya, wawili hao ni pacha halisi huku Bi Rosemary Khaveleli akiwa mama yao halisi.

Matokeo hayo, hata hivyo, yalionyesha kuwa msichana Mevis Imbaya, aliyekuwa akiishi na Melon, si dada yao halisi.

Ripoti ilibaini kuwa mamake Mevis ni Bi Angeline Omina, aliyekuwa akiishi na Sharon katika mtaa wa Kangemi, Kaunti ya Nairobi.

“Chembechembe zao za DNA zinalingana kwa asilimia 100, hali inayothibitisha kuwa ni pacha halisi,” ilisema ripoti hiyo.

Uchunguzi huo uliendeshwa na Dkt Ahmed Kalebi kutoka maabara ya Lancet. Pacha hao walitenganishwa katika hali tatanishi mnamo 1999 mara tu baada ya kuzaliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kakamega.

Wawili hao waliungana mnamo Aprili kupitia mtandao wa Facebook miaka 19 baada ya kuishi katika makazi na maisha tofauti. Kwenye mahojiano ya awali, Bi Khaveleli alisema kwamba alikuwa ameenda kujifungua watoto watatu, lakini baada ya kufanyiwa upasuaji, wauguzi walimwambia kwamba alijifungua pacha.

“Nilijifungua watoto wawili mnamo Agosti 15, 1999, wakati mimba yangu ilipokuwa imedumu kwa miezi minane na nusu,” akasema.

Mabadiliko

Hali ilianza kubadilika mnamo 2018, baada ya Melon na wanafunzi wenzake kuzuru Shule ya Upili ya Wasichana ya Shikoti (anakosomea Sharon) ambapo wanafunzi walishangazwa na mfanano wa maumbile yake na Sharon.

Wanafunzi hao hata hivyo walimwambia kuwa ana dada yake katika shule hiyo, lakini akakataa, akisema kuwa dada yake wa pekee aliye naye anasoma katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kimosin.

Wawili hao hawakufanikiwa kukutana siku hiyo.