Habari Mseto

Uchuuzi marufuku katika mitaa iliyofungwa

May 10th, 2020 1 min read

VALENTINE OBARA na WACHIRA MWANGI

SERIKALI imezidisha masharti kwa wakazi wa mitaa ya Old Town mjini Mombasa, na Eastleigh katika Kaunti ya Nairobi kwa juhudi za kuepusha ueneaji virusi vya corona.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman, alisema Jumamosi serikali imeamua kupiga marufuku uchuuzi katika mitaa hiyo miwili.

Hii ni pamoja na masharti yaliyotolewa awali kwa maeneo hayo ambayo yalifungwa na serikali kwa siku 15, ikiwemo kufunga majengo ya kibiashara, masoko na kuzuia watu kukusanyika eneo moja.

“Tunaomba wakazi wa maeneo hayo waendelee kufuata maagizo yanayotolewa kwao ili kusaidia kurudisha hali ya kawaida,” akasema.

Mitaa hiyo miwili ilifungwa baada ya idadi ya maambukizi kuongezeka kwa kasi katika siku chache zilizopita.

Katika mtaa wa Old Town, maji yalizidi unga wakati wakazi walikataa kupimwa kama wameambukizwa virusi vya corona, na wengine wao wakatoroka.

Jumamosi, hali tofauti na ile ya Old Town ilionekana katika mtaa wa Tudor, eneobunge la Mvita wakazi walipojitokeza kwa wingi kupimwa ikiwa wameambukizwa.

Wakazi wa mtaa huo walisema wanatambua hatari iliyopo na njia ya busara ni kutambua kama wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Walianza kuwasili alfajiri katika Shule ya Msingi ya Marycliff hata kabla maafisa wa Wizara ya Afya kuwasili kwa shughuli hiyo.

Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, alisema shughuli ya kupima watu kwa wingi inaendelezwa pia katika maeneo ya Ganjoni na Majengo.

Maeneo mengine ya kaunti hiyo ambapo kuna idadi kubwa ya maambukizi ni Likoni na Nyali.