UDA chajiuza kama chama kisichobagua Mkenya yeyote

UDA chajiuza kama chama kisichobagua Mkenya yeyote

Na LEONARD ONYANGO

WANDANI wa Naibu wa Rais William Ruto wametangaza kuwa wameanza harakati za kutumia chama cha United Democratic Alliance (UDA) kubomoa Jubilee.

Wakiongozwa na aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen na aliyekuwa naibu Kiranja wa Wengi katika Seneti Susan Kihika, viongozi hao Ijumaa wamewataka wafuasi wa Jubilee kuhamia chama cha UDA ambacho wamedai kuwa hakina ubaguzi.

Wamesema walilazimika kuhamia katika chama cha UDA baada ya kutengwa na kupigwa marufuku kuenda katika makao makuu ya chama cha Jubilee.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza wakati wa kutoa vyeti kwa wawaniaji wa kiti cha ugavana wa Kaunti ya Nairobi, ubunge katika maeneobunge ya Kabuchai na Matungu; na Wadi za Kiamokama (Kisii), London (Nakuru) na Hells Gate (Nakuru).

Askofu Margaret Wanjiru amekabidhiwa tiketi ya chama cha UDA kuwania ugavana katika Kaunti ya Nairobi katika uchaguzi mdogo uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 18, 2021.

Uchaguzi huo mdogo ulisitishwa kwa muda baada ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuenda kortini kupinga kutimuliwa kwake na Seneti hadi pale kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Lakini Ijumaa, viongozi wa ‘Tangatanga’ wamedai kuwa kesi ya Bw Sonko ni njama ya serikali ya Jubilee kuchelewesha uchaguzi mdogo wa Nairobi ‘baada ya kuhofia kuwa watabwagwa na mwaniaji wa UDA’.

Askofu Wanjiru sasa atamenyana na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru anayepigiwa upatu kupeperusha bendera ya Jubilee.

Chama hicho pia kimekabidhi tiketi Bw Evans Kakai Masinde na Bw Alex Lanya kuwania ubunge katika maeneobunge ya Kabuchai na Matungu mtawalia.

Maeneobunge hayo yalisalia wazi baada ya vifo vya Justus Murunga (Matungu) na James Lusweti (Kabuchai).

Hatua ya UDA kusimamisha wawaniaji wake inamaanisha kuwa Dkt Ruto atakuwa anaendesha kampeni dhidi ya wawaniaji wa Jubilee na huenda akamenyana na Rais Uhuru Kenyatta katika kampeni haswa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi.

Hatua hiyo pia ina maana kwamba Naibu wa Rais Ruto amepuuzilia mbali ombi la viongozi wa chama cha Amani National Congress chake Musalia Mudavadi na Ford Kenya kinachoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula ambao walimtaka asisimamishe wawaniaji katika chaguzi ndogo za Matungu na Kabuchai.

Wakizungumza Alhamisi katika ibada ya kumuaga Mama Hannah Mudavadi, mama ya kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi jijini Nairobi, viongozi wa ANC na Ford Kenya walimsihi kiongozi wa ODM Raila Odinga na Dkt Ruto wasisimamishe wawaniaji wao katika chaguzi hizo ndogo.

Chama hicho cha Wilibaro pia kilitoa tikiti kwa wawaniaji wa udiwani Antony Wachira (London), Jonathan Warothe (Hells Gate) na Moses Nyakeramba (Kiamakoma).

“Wawaniaji wetu wote watakuwa wanatumia chama cha UDA kuanzia sasa. Sisi hatuogopi kujihusisha na UDA kwa sababu hata wao (viongozi wa Jubilee) wamekuwa wakijihusisha na shughuli za chama cha ODM bila kuadhibiwa. Kadhalika, chama cha Party for Development Reform (PDR) kilichobadilisha jina lake kuwa UDA kilikuwa mshirika wa Jubilee na hivyo basi hatujakiuka sheria,” akasema Bw Murkomen.

Wanasiasa sasa wako huru kutumia chama hicho cha ‘Wilibaro’ kuwania viti katika chaguzi mbalimbali baada ya watu kukosa kuwasilisha pingamizi dhidi ya chama hicho kinachohusishwa na Naibu wa Rais William Ruto.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Ann Nderitu, mapema wiki hii alisema hakuna mtu aliyejitokeza kupinga hatua ya chama cha Party for Development Reform (PDR) kubadili jina lake kuwa United Democratic Alliance (UDA).

Bi Nderitu pia alisema kuwa afisi yake haijapokea pingamizi za kutaka kuzuia chama cha UDA kutumia nembo ya ‘Wilibaro’ au kaulimbiu yake ya ‘Kazi ni Kazi’.

UDA inayoongozwa na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama, ni kati ya vyama sita ambavyo Naibu wa Rais Ruto analenga kutumia kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Vyama vingine ambavyo Dkt Ruto analenga kutumia ni The Service Party (TSP) cha aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, New Democrats kinachohusishwa na aliyekuwa mbunge David Kiprono Sudi na People’s Empowerment Party (PEP) kinachohusishwa na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Vingine ni The United Green Party (UGP) na Grand Dream Development Party (GDDP).

You can share this post!

Joho ataka Raila aunge Mpwani kuwania urais

Arsenal wamsajili chipukizi matata Omar Rekik kutoka Hertha...