Habari za Kitaifa

UDA, JUBILEE, ODM, WIPER kuandaa chaguzi 2024 kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027

January 7th, 2024 2 min read

WANDERI KAMAU NA CHARLES WASONGA

VYAMA vikuu vya kisiasa vimeanza mipango kabambe kuwasajili wanachama wake kote nchini.

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Rais William Ruto, Orange Democratic Movement (ODM) chake Bw Raila Odinga na Jubilee, chake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, vimeanza mwaka mpya (2024) kwa uzinduzi mkubwa shughuli za usajili wa wanachama katika sehemu tofauti nchini.

Upeo wa usajili wa wanachama wapya katika vyama vya UDA na ODM utakuwa ni maandalizi ya chaguzi za mashinani, zilizopangiwa kufanyika Aprili.

UDA ilikuwa imepanga kuandaa chaguzi zake Desemba 2023, lakini ikaahirisha zoezi hilo bila kutoa sababu zozote.

Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, pia ametangaza mipango ya kuanza zoezi hilo, hatua inayoonekana kuwa juhudi za kujitayarisha kutwaa nafasi ya mgombea urais wa mrengo wa Azimio la Umoja.

Bw Musyoka analenga kuimarisha ngome yake ya kisiasa kama mkakati wa kuhakikisha hatalazimishwa kumuunga mkono kiongozi yeyote katika upinzani, kwenye Uchaguzi Mkuu 2027.

Tayari, Bw Musyoka ameshatangaza kwamba itakuwa heri kwake kustaafu kutoka siasa badala ya kutowania urais mara nyingine.

“Nitazunguka kila sehemu nchini mwaka huu. Hivyo, mwaka huu utakuwa muhimu sana kwa demokrasia nchini. Jitayarisheni kwa shughuli nyingi; shughuli za kisiasa na zinazowahusu raia,” akasema Bw Musyoka, kwenye mahojiano na ‘Taifa Jumapili’ majuzi.

Mnamo Jumatano, Bw Odinga alitangaza kwamba ODM itaandaa chaguzi zake hapo Aprili.

Kwa sasa, Bw Odinga yuko jijini Mombasa, ambako amekuwa akifanya mikutano tofauti na maafisa wakuu wa chama hicho.

Chama hicho kimekuwa kikiendesha shughuli za kusajili wanachama wake katika maeneo tofauti nchini. Maafisa wake wamekuwa wakitaja zoezi hilo kama mpango wa muda mrefu wa kukipa nguvu chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

“Tuko kwenye mchakato wa kuwasajili wanachama. Mnajua kwamba chama chetu kimekuwa kikiandaa chaguzi zake kila baada ya miaka mitano, hivyo basi usajili wa wanachama ni jambo ambalo limekuwa likiendelea. Tulianza zoezi hilo mnamo Novemba na tutaendelea hadi Machi mwaka huu,” akasema Bw Odinga, kwenye kikao na wanahabari jijini Mombasa.

“Tutaandaa chaguzi za chama chetu Aprili 2024. Baadaye, tutaandaa Kikao cha Kitaifa cha Wajumbe (NDC) kati ya Mei na Juni mwaka huu,” akasema.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Bw Opiyo Wandayi, alisema kuwa mpango huo ni mkakati wa kukiweka chama hicho katika nafasi ambapo kitaonekana kama mwokozi pekee wa Wakenya, hasa vijana, wanaohisi “kusahauliwa” na uongozi uliopo.

“Zoezi la kusajili wanachama limepata uungwaji mkono mkubwa, hasa kutoka kwa vijana, wanaotaka kujitambulisha na ODM. Hiki ndicho chama pekee kinachojulikana kuwa na maono makubwa,” akasema Bw Wandayi, kwenye mahojiano na ‘Taifa Jumapili’.