UDA ni chama cha mahasla – Ruto

UDA ni chama cha mahasla – Ruto

Na SAMMY WAWERU

NAIBU wa Rais William Ruto ametetea hatua ya kubuniwa kwa United Democratic Alliance (UDA), chama anachosema ni cha ‘mahasla’.

Hastla, ni nembo ambayo amekuwa akiitumia kushwishi wananchi maskini katika mchakato wake kusaka kura kuingia Ikulu 2022, kwa msingi kuwa sera zake zinalenga kuinua maisha ya Wakenya.

Kulingana na Dkt Ruto, chama cha UDA, kinachohusishwa naye ni cha kitaifa anachohoji kitasaidia kuzima siasa za kikabila, baada ya 2022 endapo atakuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya.

Kwenye mahojiano na runinga ya Inooro, inayopeperusha matangazo kwa lugha ya Kikuyu, maelezo ya Naibu Rais yaliashiria amegura chama tawala cha Jubilee.

Katika uchaguzi mkuu wa 2017, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais Ruto walihifadhi nyadhifa zao kupitia mrengo wa Jubilee, uliobuniwa na wawili hao baada ya kuvunja vyama walivyotumia 2013.

Dkt Ruto alisema sababu kuu za kubuni UDA, ni kutokana na Jubilee (JP) kutekwa nyara na baadhi ya viongozi na wasiasa aliodai ni ‘matapeli’.

“JP imetekwa nyara na matapeli na ndio maana tunajipanga na njia nyingine,” akasema.

Naibu Rais aidha alisema Jubilee imetwaliwa na upinzani, baada ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa Machi 2018, kupitia mapatano ya Handisheki.

“Tumeibuka na UDA kukomboa taifa na uchumi,” akaelezea, akipigia upatu chama hicho alichodai kina sura ya kitaifa.

You can share this post!

Ujenzi wa daraja Starehe kucheleweshwa

FAUSTINE NGILA: Tuna kibarua kukuza miji ya kibiashara na...