UDA yapinga talaka

UDA yapinga talaka

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, kimepinga uamuzi wa Jubilee kutaka muungano uvunjwe kutokana na tofauti za kifalsafa kati ya vyama hivyo viwili.

Kwenye barua aliyomwandikia Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu, Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina alisema wanapinga uamuzi huo wa Jubilee kwa sababu ulichukuliwa bila mashauriano na asasi husika za vyama hivyo viwili.

“UDA inapinga uamuzi huo wa Jubilee kwa misingi ya sehemu ya 10 (4) ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2012 na Kipengele cha 6 cha Mkataba wa Muungano. Asasi husika za vyama tanzu zitachukua hatua mwafaka za kusuluhisha mzozo huo na utajulishwa kuhusu matokeo,” Bi Maina akasema kwenye barua aliyomwandikia Bi Nderitu.

Katibu mkuu wa UDA amechukua hatua hiyo siku mbili baada ya chama cha Jubilee kuanzisha mchakato kukatiza uhusiano wake na chama hicho ambacho zamani kilijulikana kama Party of Development and Reform (PDR).

Katika barua aliyomwandikia Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Nderitu, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alisema Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) ya Jubilee iliamua kuwa itakuwa vugumu kukamilisha muungano kati yake na PDR baada ya chama hicho kubadili “jina, nembo, maafisa na sera”.

“Maafisa wote wa PDR waliokuwa wakishiriki katika mazungumzo kuhusu muungano wameondolewa na wale wapya wamedhihirisha uadui na Jubilee kwa kudhamini wagombeaji nje ya kaunti ambazo zililengwa ushirikiano wetu ulipoanza kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017,” akasema Bw Tuju.

Jubilee pia ilipinga kauli mbiu ya Hasla ambayo inaendelezwa na UDA.

Chama hicho tawala kilisemakwamba kauli hiyo inakwenda kinyume na kauli yake ya ‘Tuko Pamoja’ ambayo inadhamiria kuunganisha nchi.

Baadhi ya wanachama wa UDA pia wamekuwa wakilaumiwa kwa kudhamini wagombeaji kupinga wale wa Jubilee katika chaguzi ndogo zilizofanyika katika wadi za London na Hellsgate (Nakuru) na katika uchaguzi mdogo ujao katika eneobunge la Bonchari (Kisii).

Kulingana na mkataba kati ya Jubilee na PDR mnamo Mei, 2017, PDR ingedhamini wagombeaji katika kaunti za Pokot Magharibi, Isiolo, Mandera, Wajir na Garissa.

Wiki jana Naibu Rais Dkt Ruto alikariri kuwa atatumia UDA kuwania urais 2022 kwa sababu ndicho chama ambacho kinashirikiana na Jubilee, endapo hali ya uthabiti haitarejeshwa ndani ya chama hicho tawala.

“Bado nina matumaini kwamba tunaweza kukomboa Jubilee na kuiweka katika mkondo wa maono yake ya awali. Ikiwa hilo haitawezekana, tuko na mpango mbadala. Tuko na chama dada ambacho sasa kinaitwa UDA. Ikiwa mambo yataenda mrama Jubilee, chaguo letu mwafaka litakuwa UDA,” akasema kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen Alhamisi wiki iliyopita.

You can share this post!

Wanaodai Magufuli aliuawa kwa sumu wajitokeze – Rais...

Ampotosha Rais?