UDA yataka Matiang’i achunguze vurugu

UDA yataka Matiang’i achunguze vurugu

Na MERCY SIMIYU

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA), kimeitaka Wizara ya Usalama kuhakikisha kuwa waliochochea ghasia zilizovuruga mkutano wa Naibu Rais William Ruto Jumapili jijini Nairobi, wanaadhibiwa.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bw Johnstone Muthama na Katibu Mkuu, Bi Veronica Maina, pia walitaka polisi kuwakamata wahuni hao waliodai walikuwa wafuasi wa ODM.

“Wakenya wanasubiri kuona ikiwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, ambaye ameunga mkono azma ya urais ya Raila Odinga, ataweka kando kofia yake ya kisiasa na kuwaokoa Wakenya kutokana na ghasia zinazoendelezwa na mwanasiasa huyu,” Bw Muthama akasema kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya UDA, Nairobi.

Naye Bi Maina akasema: “Sasa ni wazi kwamba Raila anataka kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu ujao ziendeshwe katika mazingira ya fujo, vitisho na makabiliano. Anachochea fujo ilhali yeye anapewa ulinzi na serikali kwa sababu ya handisheki.”

Maafisa hao walimtaka Bw Odinga kukoma kujificha nyuma ya maridhiano ya kisiasa kati yake na Rais Uhuru Kenyatta na ulinzi wa serikali kuendeleza fujo nchini.

Baada ya fujo kushuhudiwa katika mkutano uliofanyika uwanja wa Jacaranda, eneo bunge la Embakasi Mashariki, Dkt Ruto alimsuta Bw Odinga akidai ndiye aliyewatuma wafuasi wake kuuvuruga.

“Wewe mtu wa kitendawili, ni mtu aliyetenda kosa la uhaini. Hauwezi kututisha. Usidhani kwamba unaweza kutisha kila mtu, kila mahali. Hizi ni siku zako za mwisho,” Dkt Ruto akafoka.

“Tunakueleza kutoka hapa Jacaranda kwamba ewe unayejulikana kwa kuchochea fujo na kujiapisha na kukataa matokeo ya uchaguzi, siku zako zimehesabiwa,” akaongeza.

Lakini Bw Odinga alipuuzilia mbali madai hayo ya Dkt Ruto akidai ndiye aliwadhamini waliovuruga mkutano wake ili amsingizie yeye (Bw Odinga).

“Ruto anajulikana kwa kuvuruga mikutano yake. Ruto anajulikana kwa kuendeleza siasa za fujo tangu alipoingia katika siasa kwa mara ya kwanza kupitia kundi la YK92,” Bw Odinga akasema kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na msemaji wake, Bw Dennis Onyango.

Bw Onyango alisema kuwa walikuwa na habari kwamba vijana walikuwa wakilipwa kuhudhuria mkutano huo.

Lakini jana, Mbw Muthama na Bi Maina, walishikilia kuwa magenge ambayo yalivuruga mkutano wa kampeni wa Dkt Ruto, walikuwa wafuasi wa Bw Odinga.

“Hii sio mara ya kwanza kwa Bw Odinga kutumia wahuni wa ODM kuzua fujo katika mkutano ya Dkt Ruto. Mnamo Septemba 5, 2021 msafara wa Naibu Rais ulishambuliwa kwa mawe katika eneo bunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri. Na miezi miwili baadaye, wahuni wa ODM kwa mara nyingine walivuruga mkutano wake kwa njia hiyo hiyo kule Kondele, Kaunti ya Kisumu,” akasema Bw Muthama.

Mkutano huo ulikuwa wa tatu kuongozwa na Dkt Ruto jijini Nairobi kuuza sera zake akijipigia debe katika safari yake ya kuingia Ikulu kupitia uchaguzi mkuu mwaka huu.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wataka CBC iondolewe, wasema ni ghali kwa wazazi na...

TUSIJE TUKASAHAU: OKA yaelekea kuzikwa, haitambuliwi...

T L