Makala

Udadisi wa vita vya kibiashara kati ya Amerika na China

August 2nd, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

KWA miaka kadhaa sasa, Amerika na China zimekuwa katika malumbano makali ya ubabe wa kibiashara na uwezo wa kijumla.

Amerika imekuwa na wasiwasi mkuu kuhusu jinsi China hujishindia biashara katika mataifa limbukeni hasa ya Afrika na ambapo Amerika ilikuwa tangu jadi ikiunda faida si haba kupitia kuyafadhili kwa mikopo na kutwaa kandarasai za ujenzi wa miundombinu.

Hata hivyo, Amerika imejipata hoi katika biashara ulimwenguni ambapo China inazidi kutawala kupitia mikopo na ujuzi wa ujenzi na pia kile wengine wanasema ni mfumo wa kupata biashara kupitia ukuruba wa wanasera wa mataifa mengi duniani.

Kwa sasa, Rais Donald Trump ametangaza kuwa ataweka vikwazo katika biashara za China nchini mwake hasa kupitia kuzigonga kwa ushuru wa juu.

Amesema kuwa kuanzia Septemba, karibu bidhaa zote ambazo huuzwa katika taifa lake zikiwa na asili ya Kichina zitakuwa zikitozwa ushuru wa ziada wa asilimia 10.

Ina maana kuwa China sasa itaanza kulipa ushuru wa ziada wa kiasi cha Dola 300 bilioni kwa mwaka na hivyo basi kupisha enzi mpya ya biashara ya vikwazo katika soko la Amerika ikiathiri China.

Bidhaa ambazo Trump ameorodhesha kama za dharura katika ushuru huo wa ziada ni pamoja na vinyago, nguo, viatu, bidhaa za simu na zile zote zingine za kieletroniki hali ambayo Trump katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii ameitaja kama “adhabu ya kulainisha biashara.”

Ni hivi karibuni ambapo Trump alitangaza vikwazo kwa kampuni ya Huawei akisema kuwa imepambwa na mitambo ya ujasusi hivyo basi kuinyima usajili katika taifa la Amerika na Google kulazimika kutoiruhusu kutumia programu au Apps zenye umaarufu mkubwa duniani.

“Hatujaafikiana kuhusu biashara ya kutufaa kwa kiwango cha 50:50 kati ya Amerika na China kwa sababu haijatekeleza mazungumzo ya kununua bidhaa nyingi za Amerika, lakini imezidi kuingiza bidhaa zake katika soko la Amerika. Bila vikwazo vya kiushuru ndio tunufaike kama uchumi wa Amerika, hakuna manufaa yoyote ya kuwa waandalizi wa soko la bidhaa za Kichina,” akateta Trump.

Kinaya

Hata hivyo, Trump amesisitiza kuwa hakuna athari za kibinafsi kati yake na Rais wa China, Xi Jinping na pia uhusiano kati ya Amerika na China kama mataifa “utabakia ule wa urafiki na ushirika.”

Hayo ni matamshi ambayo yametajwa tu kuwa ya demokrasia, wengi wakisema kuwa “hivi ni vita kamili vya kibiashara ambayo inashirikishwa na Trump dhidi ya China kwa msingi wa ubabe wa ushawishi katika ulingo wa kibiashara kote duniani.”

Mtaalamu wa masuala ya biashara za kimataifa, Shedrack Kariuki anasema kuwa “usidanganywe na usifumbwe macho kwa kuwa huu ni mwanzo wa vita baridi vya kiuchumi kati ya mataifa mawili yaliyuo na ushawishi mkuu.”

Anasema China itajibu mipigo kupitia kuwekeza zaidi katika mataifa ya Asia na Afrika na kutwaa soko la Amerika kwa kiwango kikuu.

“Pia, kuna kampuni tele za Amerika ambazo hutegemea ujuzi, utaalamu na soko katika taifa la China na washirika wake. China pia ina ushawishi katika mataifa mengine hasa ya Asia. China nayo ikitangaza vikwazo vyake na ianze kuhamisha kampuni zake kutoka Amerika, nayo Amerika itaumia,” anasema Bw Kariuki.

Katika hali hiyo, Bw Kariuki anasema kuwa kampuni ya China na yale ya Amerika huenda yazidishe malumbano yakifuata sera za marais wao dhidi ya mwingine katika vita hivi.

“Lakini cha maana ni kujua wateja ndio wataumia zaidi hasa wale wa Amerika kwa sasa kwa kuwa bidhaa za China zitazidi kuwa za bei za juu ili kukumbatia sera hii mpya ya ushuru. Katika hali hii, Amerika kama kiongozi katika uchumi wa kitaifa itapata ushuru wa juu nao wananchi wake wapoteze uwezo wa kuweka akiba katika mfumkobei na hatimaye wapungukiwe na uwezo wa ujasiariamali na uthabiti katika utajiri. Katika hali hiyo, Trump huenda akashinda lakini Amerika ikapoteza,” anasema Bw Kariuki.