Makala

UDAKU: Difenda Tomori Fikayo na msupa Geordie Amber Gill wawasha moto wa mapenzi

March 2nd, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

MSHINDI wa zamani wa taji la Love Island, Geordie Amber Gill, 24, amefichua kwamba amepata hifadhi jipya moyoni mwa mwanasoka matata wa Chelsea, Tomori Fikayo.

Mwishoni mwa wiki jana, Amber alipakia kwenye mtandao wake wa Instagram picha alizowahi kupigwa pamoja na Fikayo, 22, wakila raha ya ujana katika ufuo wa Ibiza.

Kwa mujibu wa kipusa huyo, Fikayo, ambaye anachezea timu ya taifa ya Uingereza, amewahi kulitikisa buyu lake la asali mara mbili jijini London, Uingereza.

Aidha, alisema ziara yao ya hivi karibuni nchini Uhispania ilipania kuwapa jukwaa la kutafuta mtoto atakayekoleza kabisa penzi lao.

Amber anaanza kutoka kimapenzi na Fikayo miezi mitano baada ya kuagana rasmi na mwanaraga mahiri wa Ireland, Greg O’Shea mnamo Septemba 2019 kutokana na jicho kali la nje la kidume hicho.

Fikayo aliwahi kukiri kwamba anawaniwa pakubwa na makahaba wakongwe mitandaoni.

Amekuwa na uhakika wa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Chelsea msimu huu tangu arejee kutoka Derby County, iliyojivunia huduma zake kwa mkopo wa msimu mmoja mnamo 2018-19.

Fikayo aliwajibishwa na timu ya taifa ya Uingereza kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2019 katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Euro 2020 dhidi ya Kosovo.

Alikichochea kikosi hicho cha kocha Gareth Southgate kusajili ushindi wa 4-0.

Katika mahojiano na gazeti la The Sun wiki iliyopita, Amber alikiri kwamba alihamia jijini London mwishoni mwa mwaka 2019 kwa nia ya kusaka dume litakalofufua hisia zake za mapenzi zilizozimwa ghafla na O’Shea.

Kabla ya kuanza kutambaliwa na O’Shea, Amber alikuwa kidege cha mwigizaji maarufu Jamie Lomas anayemzidi umri kwa miaka 24.