Makala

UDAKU: Fanny: Lukaku, Balotelli waihujumu ndoa yangu

October 21st, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WIKI chache baada ya mrembo Fanny Neguesha kumtaka mwanasoka Mario Balotelli kumkoma kabisa, mwanamitindo huyo wa Ubelgiji amefichua kwamba ndoa kati yake na kiungo Mario Lemina wa Southampton inayumbishwa na mawimbi mapya. Lemina kwa sasa anaichezea Galatasaray ya Uturuki kwa mkopo.

Hii ni baada ya kichuna huyo mwenye umri wa miaka 29 kukiri kunyemelewa mitandaoni na wanasoka walioagana majuzi na Manchester United ambao kwa mtazamo wake, wana nia ya kumvurugia ndoa.

Kulingana naye; Romelu Lukaku na Alexis Sanchez wamekuwa wakilihemea pakubwa penzi lake kwa kurusha picha na jumbe za kumtia kishawishini aachane na Lemina tangu mumewe huyo aanze kuhusishwa na uwezekano wa kuhamia uwanjani Old Trafford muhula huu.

Katika mahojiano yake na gazeti la ‘The Sun’ wiki jana, Neguesha aliungama kwamba wengi wa wanaume wanaomvizia ni wachezaji wa Man-Utd ambao walimfahamu wakati alipokuwa akitoka kimapenzi na Balotelli aliyekuwa sogora wa Manchester City. Madai ya Neguesha yanajiri mwezi mmoja baada ya kuungama kwamba Balotelli amekuwa akiwania fursa ya kuanza kulitikisa upya buyu lake la asali.

“Ana namba nyingi za simu. Mara anatuma ujumbe, mara anapiga simu, mara anarusha picha. Nahofia hili litaanza kumkera Lemina ambaye amenivumilia sana,” akasema kwa kusisitiza kwamba sasa haoni sababu yoyote ya mumewe kutua Old Trafford iwapo hali itakuwa hivyo jijini Manchester.

Uamuzi wa Balotelli kuliwania tena tunda la Neguesha ulichochewa na hatua ya kichuna huyo kuusifia utenda-kazi wa nyota huyo kila walipokuwa wakishiriki miereka ya faraghani hapo awali.

Katika mojawapo ya kauli zake, alisema bado hajampata fundi wa mahaba anayemzidi Balotelli kwa ujuzi wa kukitalii kisima chake cha maji makuu.

“Balotelli si dume linalotisha uwanjani pekee. Pia ni gwiji wa mechi za chumbani. Sijaona kati ya wote waliowahi kumenya tunda hili, anayeweza kukifikia kiwango cha fowadi huyo. Ingawa hivyo, kwa sasa nimepania kutulia katika ndoa ili nimzalie Lemina watoto zaidi,” akasema.

Kwa pamoja na Lemina, videge hao wamejaliwa mtoto wa kiume: Isiah-King.

Neguesha ambaye ana historia ya kuwa mwepesi wa kujilegeza kimapenzi kwa wanasoka maarufu wenye vipochi vinono kihela, sasa anamtaka mumewe ajiunge na Arsenal baada ya kipindi chake cha mkopo kambini Galatasaray kutamatika.

Neguesha alitemana na Balotelli mnamo 2014 baada ya kuhusiana kwa miezi 18. Mbali na Balotelli, Neguesha amewahi pia kutoka kimapenzi na kiungo wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Senegal, Cheikhou Kouyate, 29, na mwanamuziki mzawa wa Canada, Aubrey Drake, 33.