Michezo

UDAKU: Hudson-Odoi avunja sheria za kuzuia virusi vya corona kwa sababu ya kichuna

May 18th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

CALLUM Hudson-Odoi anatarajiwa kukosa mazoezi ya kwanza ya vikundi vidogo vya wachezaji yatakayoanza Mei 19 baada ya kuvunja sheria za kutotangamana na watu wakati huu wa janga la virusi hatari vya corona.

Winga huyu mwenye umri wa miaka 19, ambaye alipatikana na virusi hivyo mwezi Machi kabla ya kupona mapema Aprili, alikamatwa Mei 17 asubuhi baada ya kualika mwanamke nyumbani kwake.

Mwanamke huyo, ambaye anasemekana alifika kwa Hudson-Odoi mnamo Mei 17 jioni, aliwahiwa hospitali kwa sababu alikuwa akihisi vibaya.

Gazeti la The Sun lilidai kuwa mwanamke aliyekuwa na Hudson-Odoi ni mwanamtindo, ambaye walikutana naye mtandaoni na kisha kualikwa.

Hudson-Odoi huenda akaadhiwa vikali na klabu yake kwa kuifanya ionekane vibaya, hasa baada ya klabu hiyo kuonyesha kimejituma zaidi katika vita dhidi ya maambukizi ya corona.

Mchezaji huyu mwenye asili ya Ghana hulipwa mshahara wa Sh23.4 milioni kila wiki uwanjani Stamford Bridge.