UDAKU: Huyu Neymar hapoi, amedakia Bruna kabla Natalia kupiga baibai

UDAKU: Huyu Neymar hapoi, amedakia Bruna kabla Natalia kupiga baibai

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI matata wa Paris Saint-Germain (PSG), Neymar Jr, ameanza kumumunya mwanamitindo maarufu wa Brazil, Bruna Biancardi.

Wawili hao walionekana wakiponda raha katika ufuo wa Ibiza nchini Uhispania juma lililopita.

Neymar, 29, alichukua fursa hiyo kumtambulisha Biancardi, 27, kwa baadhi ya marafiki na familia zao.

Kidosho huyo baadaye alipakia mtandaoni picha alizopigwa na Neymar huku wakilishana mabusu motomoto.

Picha hizo zilichangamkiwa na maelfu ya mashabiki wa Biancardi kwenye Instagram.

Kichuna huyo alikuwa miongoni mwa wanamitindo waliohudhuria dhifa ya kufunga mwaka wa 2020, iliyoandaliwa na Neymar jijini Rio de Janeiro, Brazil.

“Naamini kilele cha urafiki huu ni ndoa. Ni suala la muda tu,” akaandika Biancardi.

Kwa upande wake, Neymar alisema: “Nakupenda kwa moyo wangu wote. Mimi huamini miujiza ya mwanzo bora katika kila jambo jipya.”

Neymar anafichua mipango yake na Biancardi wiki chache baada ya mchumba wake wa zamani, Natalia Barulich, kumtaka aharakishe kumfanya wake wa halali.

“Acha mwendo wa kobe; fanya hima urasimishe mambo kabla nikufyatulie watoto,” aliandika Natalia, 29, mtandaoni huku akitia emoji za mabusu mwishoni mwa ujumbe.

Natalia alianza kumburudisha Neymar chumbani Februari 2020, miezi sita baada ya kipusa huyo kutemana na mumewe wa miaka miwili, Juan Luis Arias.

Tangu Neymar atemane na mwigizaji raia wa Brazil, Bruna Marquezine, sogora huyo ametoka kimapenzi na vidosho wa kila sampuli.

, akiwemo mwanahabari raia wa Uhispania, Melodie Penalver.

Amewahi pia kuchovya asali kwenye mizinga ya warembo Emilia Mernes, Liza Brito, Danna Paola, Mari Tavares, Larissa de Macedo Machado almaarufu Anitta na Ellen Santana aliyetawazwa mshindi wa Miss BumBum nchini Brazil mnamo 2018.

Penzi la Neymar limewahi pia kuwaniwa na vipusa Giovanna Lancelotti, Sabine Jemeljanova, Selena Gomez, Soraja Vucelic, Chloe Grace Moretz, Noa Saez, Izabel Goulart na Alsessandra Ambrosio.

Neymar ana mtoto mmoja wa kiume – Davi Lucca da Silva Santos aliyezaliwa na mrembo raia wa Brazil Carolina Dantas, 27, mnamo Agosti 24, 2011.

Mwanafasheni maarufu raia wa Italia, Chiara Nasti, amekuwa pia akimtumia Neymar video, picha na jumbe za kumtaka kimapenzi huku akimsihi mara kwa mara akutane naye ili amfichulie jinsi anavyomzimikia.

You can share this post!

DIMBA: Ruby: Beki mtulivu akiwa na boli na mkali wa...

IEBC yasema iko tayari kutii mabadiliko yoyote ya kikatiba...