Makala

UDAKU: Maguire kidume kamili baada ya mkewe kuhesabu bao jingine la mapenzi

May 10th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

DIFENDA mahiri wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Harry Maguire, 27, sasa amekuwa dume kamili baada ya mkewe Fern Hawkins kujifungua mtoto wa pili kwa jina Piper Rose.

Kimalaika hicho cha kike kinazaliwa yapata miezi tisa tangu Maguire kuagana na Leicester City na kutua ugani Old Trafford kusakatia Man-United katika uhamisho uliomfanya kuwa beki ghali zaidi duniani.

Nyota aliyesajiliwa kwa kima cha Sh11 bilioni mnamo Agosti 5, 2019 alimpiku Virgil van Dijk wa Liverpool aliyeagana na Southampton kwa Sh9.7 bilioni mnamo Januari 2018.

Lille Saint ambaye ni mtoto wa kwanza wa Maguire na Fern, alizaliwa mnamo Aprili 2019.

Msichana huyo alizaliwa miezi tisa tangu Uingereza iwachabange Colombia kupitia penalti kwenye hatua ya 16-bora ya fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Urusi mnamo 2018.

Baada ya ufanisi huo, Maguire alifunga bao lililochochea Uingereza kuwabandua Uswidi kwenye robo-fainali ila wakazidiwa maarifa na Croatia katika hatua ya nne-bora.

Maguire alimvisha Fern pete ya uchumba mnamo Februari 17, 2018 baada ya kutoka naye kimapenzi kwa zaidi ya miaka minane.

Mbali na fowadi Harry Kane wa Tottenham aliyeandika, “Hongera sana Mkubwa H,” wanasoka wengine waliompongeza Maguire kwa kujaliwa mtoto ni nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson aliyeandika “Pongezi sana Mkubwa M” kwenye mtandao wake wa Instagram.

“Nakupa mkono wa tahania mkubwa wangu. Hongera kwa mgeni mpya uliyetuletea. Pongezi kwa kazi hiyo mufti ndugu yangu,” akasema Andy Robertson aliyewahi kucheza na Maguire kambini mwa Hull City.

Kauli sawa na hizo ilitolewa pia na beki wa kushoto wa Leicester, Ben Chilwell aliyesema, “Asante sana kaka. Wewe ni zaidi ya jogoo uwanjani na chumbani. Tuendelee vivyo hivyo, tufyatue watoto tujaze dunia!”