Makala

UDAKU: Mtangazaji anayetamani kuwa mke wa pili

May 18th, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO
KICHUNA mtangazaji na Mcee anayezidi kupata umaarufu mkubwa Azeezah Hashim, hana tatizo kuwa yaya kwa watoto wa mke mwenza, ili kumruhusu kufurahia muda na mume wao.

Hii Azeezah anasema wala haiwezi kuwa ishu kwake endapo itatokea akaolewa kama mke wa pili.
Wakati mabinti wengi wa umri wake wakiona ugumu wa kuolewa kuwa mke wa pili, Azeezah anasema hilo wala halimpi taabu kabisa maana yeye kaumbwa vitofauti.
“Sina tatizo kabisa kuwa mke wa pili. Ninapotokea mimi na nilivyoumbwa mwanamume anaruhusiwa hadi wake wanne na mimi nipo radhi kuwa mke mwenza,” anasema. Azeezah alitimiza miaka 24 wiki iliyopita.
Kulingana naye, kuolewa mke wa pili ni jambo la kheri na ambalo litampunguzia presha.
“Tayari kazi ninayoifanya mimi ina presha ya kutosha halafu niongeze na presha ya mahusiano, hapana. Heri nitulize akili nikijua kama hayupo kwa Fatma basi yupo kwangu. Asipopokea simu nampigia mwenza kujua kama yupo kwake basi naendelea na shughuli zangu. Isitoshe, nipo radhi kabisa hata kuwa yaya wa watoto wa mke mwenza muradi tu, aweze kupata muda mwafaka wa kujiachia na mume wetu,” ameongeza Azeezah.