Makala

UDAKU: Ndoa ya Ronaldo pabaya visura 3 kudai kumgawia

November 2nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KATIKA hatua inayopania kuvuruga uhusiano wa kimapenzi kati ya Cristiano Ronaldo na mchumba wake Georgina Rodriguez, vipusa watatu – Rhian Sugden, 34, Ellen Santana, 22, na Erika Canela, 24, wamepasua mbarika kuhusu jinsi ambavyo wamekuwa wakitoka kimapenzi kisiri na mwanasoka huyo wa Juventus.

Kwa mujibu wa Rhian, Ronaldo ambaye ni mzawa wa Ureno alianza kumtumia jumbe za mahaba kupitia mtandao wa WhatsApp baada ya sadfa kuwakutanisha katika ufuo wa Marbella, Uhispania mwishoni mwa Septemba 2019 licha ya kwamba nyota huyo alikuwa katika ziara ya kuponda raha na demu wake Georgina.

“Alichangamkia pakubwa urembo wangu. Alianza kunisifia na akataka nimwonjeshe,” alisema Rhian akikiri jinsi ambavyo nusura jumbe za mara kwa mara alizotumiwa na Ronaldo zichangie kuvunjika kwa ndoa kati yake na mwigizaji Oliver Mellor aliyemvisha pete ya harusi mnamo Januari 2018.

Mbali na Rhian, mwanamitindo Canela aliyeibuka mshindi wa taji la Miss BumBum nchini Brazil mnamo 2017, pia ameungama kuhusu jinsi ambavyo Ronaldo amekuwa akimpangia ziara za mara kwa mara kwa minajili ya kufanikisha azma ya kutikisa buyu lake la asali.

Mnamo 2013, Ronaldo alikiri kumwendea kinyume aliyekuwa mpenzi wake Irina Shayk kwa kulimenya tunda la kidosho Andressa Urach ambaye alitawazwa malkia wa Miss BumBum mwaka huo.

“Uzito wa hisia katika arafa, video na picha za Ronaldo ziliniyeyusha nikawa mwepesi wa kumfungulia mzinga wa asali. Si siri, Ronaldo anavutiwa sana na wanawake wenye makalio makubwa, hasa washindi wa Miss BumBum,” alisema Santana kwa kufichua kwamba anatamani sana kufunga pingu za maisha na fowadi wa PSG na Brazil, Neymar badala ya kumburudisha Ronaldo.

Rhian amewahi kuhusishwa na mazoea ya kuwatia kishawishini wanasoka wa haiba kubwa pamoja na watu maarufu katika tasnia mbalimbali. Nusura aivunje ndoa kati ya mwanahabari wa BBC Radio, Vernon Kay na mkewe Tess Daly mnamo 2010 kwa kupasua mbarika kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na Kay ambao uliwekwa siri kwa miaka miwili.

Mwishoni mwa mwaka jana, wanamitindo Alexandra Mendez na Andressa Urach walitishia kufichua jumbe za kimapenzi walizokuwa wakitumiwa na Ronaldo kabla ya kukutana na Georgina ambaye kwa sasa ni mama wa mtoto mmoja.