Makala

UDAKU: Ni rasmi Usain Bolt ni baba

May 19th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

USAIN BOLT sasa ni baba baada ya Waziri Mkuu wa Jamaica Andrew Holness kutangaza Jumatatu kuwa nyota huyo wa mbio fupi amepata mtoto wa kike na mpenzi wake Kasi Bennett.

Mshindi huyo wa medali nane za Olimpiki alikuwa amefichua mwezi Machi katika karamu moja kuwa familia yao inatarajiwa kuongezeka kwa kukaribisha kimalaika.

Bolt, 33, amekuwa akichumbia Bennett, 30, tangu mwaka 2014, lakini walianika uhusiano wao kwenye umma 2016.

Bolt, ambaye ana utajiri wa Sh9.6 bilioni, ni mwanamichezo wa pili tajiri nchini Jamaica nyuma ya mchezaji wa zamani wa mpira wa vikapu Patrick Ewing (Sh29.3 bilioni).

Kasi ni mtumiaji wa mitandao ya kijamii na msanii mchoraji wa mavazi.

Ana wafuasi 345,000 kwenye mtandao wa Instagram.

Bolt, ambaye alistaafu riadha mwaka 2017 baada ya kujeruhiwa mguu mashindanoni, ana wafuasi 9.5 milioni.

Bolt anajivunia kutwaa mataji 11 ya Riadha za Dunia na ni mshikilizi wa rekodi za dunia za mbio za mita 100 (sekunde 9.58) na mita 200 (sekunde 19.19) alizoweka katika Riadha za Dunia za mwaka 2009 mjini Berlin nchini Ujerumani.