Makala

UDAKU: Ninawazia kukirudia kidege changu Bruna

October 7th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI matata wa Paris Saint-Germain (PSG) Neymar, 27, amedokeza uwezekano wa kurudiana na mchumba wake wa zamani, mwigizaji maarufu Bruna Marquezine, 23.

Hii ni baada ya mwanasoka huyo mzaliwa wa Brazil kumtaka Bruna kuzipuuza tetesi zote za hivi karibuni zilizodai kwamba kwa sasa yeye analidokoa tunda la mwanamuziki mashuhuri Larissa de Macedo Machado almaarufu Anitta, 25.

Majuzi, Neymar alihudhuria hafla moja jijini Rio, Brazil ambapo alionekana akimrushia Anitta mabusu tele hadharani. Licha ya ukaribu wao kuwasadikisha mashabiki wao kwamba wawili hao wanatoka kimapenzi, Neymar alisisitiza kwamba hapana lolote la mno kati yao; ila kwa sasa anawazia jinsi atakavyojiimarisha kitaaluma kambini mwa PSG baada ya uhamisho wake hadi Barcelona kugonga mwamba.

Ingawa hivyo, Anitta aliyehojiwa wiki jana na gazeti la The Sun, alikiri kwamba hakuna kubwa litakalomzuia kumpa Neymar funguo za mzinga wake wa asali hasa ikizingatiwa jinsi anavyotamani buyu lake litikiswe na fowadi huyo ambaye ni mwepesi wa kucheka na malango ya vichuna nje ya uwanja.

Ni kauli ambayo ilionekana kumkoroga nyongo Bruna ambaye punde alifuta picha zote za Anitta kwenye mtandao wake wa Instagram na kumnyima idhini ya kumfikia kabisa kupitia majukwaa mengine ya kijamii.

Neymar alikatiza rasmi uhusiano wake na Bruna mwishoni mwa Oktoba 2018 baada ya kuwa pamoja kwa kipindi cha miaka sita kilichotawaliwa na matukio ya kutemana na kurudiana.

Hatua hiyo iliwafungulia vipusa wengi mlango wa kuanza kuliwania peupe penzi la Neymar ambaye alionekana kutiwa kishawishini na mwigizaji maarufu mzawa wa Mexico, Danna Paola, 23.

Akiadhimisha miaka 27 ya kuzaliwa kwake, Neymar alionekana pamoja na Danna wakipigwa picha za pamoja zilizopakiwa na kidosho huyo mitandaoni.

Burudani

Danna alianza kumburudisha Neymar kimapenzi baada ya mwanasoka huyo kutemana na mwanamitindo Mari Tavares aliyejaza nafasi ya mrembo Ellen Santana aliyetawazwa mshindi wa Miss BumBum nchini Brazil mnamo 2018.

Wiki chache baada ya kumtupa Bruna, Neymar alianza pia kuamsha upya penzi lake kwa mwanamitindo Giovanna Lancelotti, 25.

Awali, alikuwa katika uhusiano mwingine wa kimapenzi na kichuna Sabine Jemeljanova ambaye amekariri kwamba yuko radhi kumpa tena Neymar tunda lake alitomase na alimenye apendavyo. Neymar ambaye ameapa kuoa mwishoni mwa mwaka ujao, amewahi pia kuonjeshwa asali na vipusa Selena Gomez na Soraja Vucelic.

Rafaella Santos ambaye ni dada yake Neymar amemshauri fowadi huyo kufanya hima na kupata hifadhi ya kudumu ya penzi lake kwa kichuna mmoja.

Kwa mujibu wa Rafaella, kakaye atapata tija zaidi na kuepushia familia yao aibu iwapo atarudiana haraka na Bruna na kuwekea uhusiano wao msingi utakaochochea ndoa imara.

Kauli ya Rafaella, 23, inatolewa miezi chache baada ya Neymar kuondolewa mashtaka ya kumbaka mwanamitindo Najila Trindale jijini Paris, Ufaransa mapema Mei 2019.