Makala

UDAKU: Nioe nikujazie dunia, kichuna amlilia Ronaldo

October 14th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPUSA Georgina Rodriguez, 25, amesema yuko tayari kumzalia Cristiano Ronaldo watoto watatu zaidi iwapo atatimiza masharti yake.

Mwanzo anataka sogora huyu wa Juventus na Ureno akome kuwasiliana mara kwa mara na wapenzi wake wa zamani wanaomtaka upya, kisha amtwae rasmi na kumfanya wake wa halali.

Katika mojawapo ya ziara zao za mara kwa mara za kutalii ufuo wa Ibiza nchini Uhispania ili kula ujana na kuponda raha, Georgina alimtajia Ronaldo kuhusu kiu aliyonayo ya kumzalia watoto zaidi ili kudhihirisha ukomavu wa penzi alilonalo kwake.

Ingawa hivyo, alimtaka mwanzo awashauri vichuna Ellen Santana, Andressa Urach, Gema Atkinson na Rosie Oliveira kumkoma kabisa. Kulingana na gazeti la ‘The Sun’, hatua hiyo ya Georgina inachochewa na matamashi ya hivi karibuni ya Katia Aveiro ambaye ni dada yake Ronaldo.

Wiki jana, Katia alidai kwamba Ronaldo si dume lenye uwezo wa kudumu na mchumba kwa muda mrefu na kuwa ana kila sababu ya kumsikitikia Georgina.

Awali, Gerogina alikuwa amepakia mitandaoni baadhi ya picha akiwa amevalia pete iliyokisiwa na wengi wa mashabiki wake kuwa ni ya uchumba. Katika mojawapo ya picha, alionekana kuketi ubavuni pa Ronaldo, ndani ya gari lao, huku akiibusu pete ya almasi aliyokuwa amevishwa kwenye chanda cha mkono wa kulia.

Ronaldo, 34, alianza kutoka kimapenzi na Georgina mnamo 2016 na kwa pamoja wamejaliwa mtoto mmoja wa kike, Alana Martina aliyezaliwa mwishoni mwa 2017.

Ingawa hivyo, Ronaldo ana watoto wengine watatu – Cristiano Jr, Eva Maria na Mateo Dos Santos.

Mapema Septemba 2019 Georgina alimtaka Ronaldo kwa mara nyingine kufanya hima na kurasimisha uhusiano wao kwa harusi.

“Sioni kitakachonizuia kumzalia Ronaldo watoto zaidi iwapo atarasimisha uhusiano uliopo kwa sasa. Mimi tayari ni mama, ila natamani kuwa mkewe halali wa ndoa, nijaze dunia pamoja naye,” akasema.

Harusi

Miezi miwili imepita tangu Dolores Aveiro ambaye ni mama yake Ronaldo, pia kumtaka mwanawe kuhalalisha uhusiano wake na Georgina kupitia harusi.

Akionekana kuridhishwa na maeko ambayo mwanawe amepata moyoni mwa Georgina, Dolores alikiri kwamba hakuwahi kuvutiwa na vichuna wa zamani waliokuwa wakiliwania penzi la Ronaldo.

Mmoja aliyetajwa na mama huyo ni kidosho Irina Shayk, mwanamitindo mwenye umri wa miaka 33 ambaye kwa sasa ni mama wa mtoto mmoja, Lea De Seine, na mke wa mwigizaji mzawa wa Amerika, Bradley Cooper, 44.