Makala

UDAKU: Rebekah Vardy kukimbilia mahakama kutafuta haki dhidi ya Coleen Rooney

June 30th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

UHASAMA kati ya wake wa wanasoka nyota Wayne Rooney na Jamie Vardy unatarajiwa kuongezeka hata zaidi baada ya Rebekah Vardy kuamua kuwa atapata haki tu dhidi ya Coleen Rooney kwa kuelekea mahakamani.

Miezi tisa baada ya Coleen kushambulia Rebekah kwenye mitandao ya kijamii akidai kuwa Rebekah alikuwa akimwanika kwenye vyombo vya habari, gazeti la Guardian linasema kuwa wawili hao wameshindwa kutatua tofauti zao nje ya mahakama.

Gazeti hilo linasema kuwa Rebekah ameshtaki Coleen katika mahakama kuu kwa kumchafulia jina na kusema kuwa msongo wa mawazo umemfanya kuwa na wasiwasi wa moyo.

Rebekah amefichua kuwa mapema mwaka 2020 alilazwa hospitalini kutokana na matusi aliyopokea mitandaoni.

Uadui wao ulianza kugonga vichwa vya habari Oktoba 2019 pale Coleen alipochapisha ujumbe mrefu kwenye mtandao wake wa Instagram akisema kwa miaka kadha sasa, kuna “mtu amekuwa akimsumbua” na aliweka mtego ambao ulimfanya kuamini kuwa Rebekah ndiye alimsababishia usumbufu huo.

Uhusiano wao uliharibika kabisa kutokana na ujumbe huo.

Rebekah ni mamaye Sofia Vardy na Ella Vardy naye Coleen amepata watoto watatu – Kit Joseph Rooney, Kai Wayne Rooney na Klay Anthony Rooney – na mumewe Wayne Rooney.