Makala

UDAKU: Ronaldo bado wima! Amfunga Georgina la 2

August 24th, 2020 2 min read

Na MWANDISHI WETU

MWANAMITINDO Georgina Rodriguez anayetoka kimapenzi na Cristiano Ronaldo, amedokeza mitandaoni kwamba amefungwa bao jingine la mahaba na mwanasoka huyo wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno.

Ronaldo tayari ana watoto wanne wakiwemo Mateo Dos Santos, Eva Maria (pacha) na Cristianinho. Ronaldo aliwapata hao katika mahusiano ya awali ya kimapenzi kabla ya Georgina kumzalia Alana Martina mnamo Februari 2019.

Mwishoni mwa mwaka wa 2019, Ronaldo alisema analenga kupata jumla ya watoto saba ili idadi hiyo iwiane na namba ya jezi yake mgongoni. Georgina sasa amewataka mashabiki wake katika mtandao wa Instagram kutarajia kumuona akianza kuhudhuria kliniki kadri anavyojiandaa kumzalia Ronaldo mtoto wa tano.

“Toto la kike,” ndiyo maneno yaliyoandikwa na kipusa huyo mzawa wa Mexico kwenye Instagram chini ya picha yake iliyokuwa na mchoro wa moyo.

Georgina alianza kumfungulia Ronaldo buyu lake la asali miaka minne iliyopita baada ya sogora huyo kutemana na mwanamitindo Cassandre Davis wa Amerika mnamo Agosti 2016.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Georgina alisema yuko tayari kumzalia Ronaldo watoto watatu zaidi ila kwa masharti. Mwanzo alitaka sogora huyo akome kuwasiliana mara kwa mara na wapenzi wake wa zamani wanaomtaka upya, kisha amtwae rasmi na kumfanya wake wa halali kwa kula yamini ya ndoa.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Georgina alimtajia Ronaldo kuhusu kiu aliyonayo ya kumzalia watoto zaidi ili kudhihirisha ukomavu wa penzi alilonalo kwake mwanzoni mwa mwaka 2020.

Hata hivyo, alimtaka mwanzo awashauri vichuna Ellen Santana, Andressa Urach, Gema Atkinson na Rosie Oliveira kumkoma kabisa.

Awali, Gerogina alikuwa amepakia mitandaoni baadhi ya picha akiwa amevalia pete iliyokisiwa na wengi wa mashabiki wake kuwa ni ya uchumba.

Katika mojawapo ya picha, alionekana kuketi ubavuni pa Ronaldo, ndani ya gari lao, huku akiibusu pete ya almasi aliyokuwa amevishwa kwenye chanda cha mkono wa kulia.

“Sioni kitakachonizuia kumzalia Ronaldo watoto zaidi iwapo atarasimisha uhusiano uliopo kwa sasa. Mimi tayari ni mama, ila natamani kuwa mkewe halali wa ndoa, nijaze dunia pamoja naye,” akasema.

Miezi mitani imepita tangu Dolores Aveiro ambaye ni mama yake Ronaldo, pia kumtaka mwanawe kuacha mwendo wa kobe na kuhalalisha uhusiano wake na Georgina kupitia harusi.