Makala

UDAKU: Tomori aambiwa ng’o! hadi pingu zifungwe

September 21st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPUSA Geordie Amber Gill, 24, amemtaka beki chipukizi wa Chelsea, Fikayo Tomori kutuliza boli na kufanikisha mipango ya ndoa kabla ya kuanza kumfunga mabao ya mapenzi.

Katika mahojiano yake na gazeti la The Sun wiki jana, Amber ambaye ni mshindi wa zamani wa taji la Love Island alikiri kwamba Tomori amekuwa akimtaka afanye hima na kumwangushia watoto.

“Nafurahi kwamba nilipata hifadhi ya penzi langu kwake. Ila naomba afanye subira hadi turasimishe uhusiano kwa kula yamini ya ndoa ndipo nimzalie vidume na mabinti,” akasema.

Awali, Amber alikuwa amepakia kwenye Instagram picha alizowahi kupigwa pamoja na Fikayo wakila raha ya ujana katika ufuo wa Ibiza, Uhispania.

Kwa mujibu wa kipusa huyo, Fikayo amekuwa akilidokoa tunda lake mara kwa mara japo akashikilia kuwa itakuwa vyema kutafuta mtoto atakayekoleza kabisa penzi lao baada ya harusi.

Amber alianza kutoka kipamenzi na Fikayo miezi mitano baada ya kuagana rasmi na mwanaraga mahiri wa Ireland, Greg O’Shea mnamo Septemba 2019.

Fikayo aliyewahi kukiri kwamba anawaniwa pakubwa na makahaba wakongwe mitandaoni, alirejea ugani Stamford Bridge mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuhudumu kambini Derby County kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Amber amekiri kwamba alihamia jijini London, Uingereza mwishoni mwa mwaka jana kwa nia ya kusaka dume ambalo lingefufua hisia zake za mapenzi zilizozimwa ghafla na O’Shea.

Kabla ya kuanza kutoka kimapenzi na O’Shea, Amber alikuwa kidege cha mwigizaji maarufu Jamie Lomas anayemzidi umri kwa miaka 23.