UDAKU: Usicheze na Georgina, mapambo yake pekee ni bei ya Toyota Prado mbili!

UDAKU: Usicheze na Georgina, mapambo yake pekee ni bei ya Toyota Prado mbili!

Na CHRIS ADUNGO

MWANAMITINDO Georgina Rodriguez, 27, ana kila sababu ya kuonea fahari uhusiano wake wa kimapenzi na Cristiano Ronaldo ambaye sasa anadumishwa kwa mshahara wa Sh74 milioni kwa wiki kambini mwa Manchester United.

Malipo hayo yatamfanya fowadi huyo raia wa Ureno kuwa mwanasoka anayedumishwa kwa ujira wa juu zaidi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Wiki jana, ilifichuka kwamba Georgina aliyewahi kuwa yaya nchini Uhispania, huvalia vito vya thamani ya zaidi ya Sh12 milioni kila anapoamua kujikwatua.

Pesa hizo zinaachana kidogo sana na kiasi cha fedha ambazo Ronaldo hulipwa kwa siku moja ugani Old Trafford.

Kidosho huyo aliyezaliwa nchini Argentina pia hupokezwa na Ronaldo kima cha Sh11 milioni kila mwezi kwa minajili ya matumizi yake binafsi.

Kwa mujibu wa gazeti la Corriere dello Sport nchini Italia, asilimia kubwa ya pesa hizo hutumiwa na Georgina kujinunulia mapambo, mavazi na vipodozi vya kila sampuli.

Vito pekee vinavyomilikiwa na demu huyo ni vya thamani ya Sh405.6 milioni.

Herini za almasi zinazovaliwa na Georgina hugharimu Sh3.1 milioni huku mkufu wake ukiwa wa Sh3.3 milioni.

Pete mbili za almasi ambazo hutia nakshi kwenye vidole vyake viwili (cha shahada na cha kati), huwa ni za Sh5.8 milioni.

Alipohudhuria tamasha ya kimataifa ya Venice Film Festival nchini Italia wiki jana, Georgina alikuwa amejipamba kwa pete nne, mkufu mmoja, vikuku na herini kutoka Giardini Segreti.

Thamani ya vito hivyo vyote ilikuwa Sh18 milioni.Ronaldo ambaye thamani ya mali yake ni zaidi ya Sh78 bilioni, alimvisha Georgina pete ya uchumba ya Sh96 milioni mnamo Septemba 2020.

Kichuna huyo sasa anajiandaa kuwa shangazi kutokana na ujauzito wa dada yake, Ivana, 31.

Japo Georgina amemzalia Ronaldo mtoto mmoja pekee – Alana Martina aliye na umri wa miaka mitatu, mrembo huyo pia ni mama mlezi wa watoto wengine watatu wa fowadi huyo wa zamani wa Juventus na Real Madrid.

Watoto hao ni Cristiano Jr, Eva Maria na Mateo Dos Santos.

Mwishoni mwa Agosti, Georgina alionekana akiwa amevalia saa aina ya Rolex, bangili na pete za almasi zenye thamani ya takriban Sh100 milioni kwenye mkono wa kushoto.

Georgina alitumia tamasha ya Venice Film kufichua kwamba yuko radhi kumzalia Ronaldo watoto watatu zaidi iwapo mwanasoka huyo atamtwaa rasmi na kumfanya wake wa halali.

Ronaldo alianza kutoka kimapenzi na Georgina mnamo 2016.

Mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021, kichuna huyo raia wa Uhispania alimtaka mvamizi huyo kufanya hima na kurasimisha uhusiano wao kupitia harusi.

You can share this post!

GUMZO LA SPOTI: Ole Gunnar alizuia mastaa 5 kuaga klabu

MBWEMBWE: Kiungo Di Maria ni mwenye guu la Almasi, ana...