Makala

Udereva si uhuni, asema mwanamke dereva wa matatu

March 16th, 2024 3 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

WANAWAKE nchini Kenya wanaendelea kupata sifa kwa jinsi wanavyojituma kufanya mambo ya kawaida kwa njia zisizo za kawaida.

Bi Mercy Ondieki, 32, ni dereva wa matatu kutoka Kisii.

Dereva huyu ni mfano bora wa wanawake ambao kama wanaume, wanahakikisha wanajenga taifa kupitia bidii kazini.

Bi Ondieki ni mmoja wa madereva wanaopendwa sana katika barabara ya Kisii-Kilgoris.

Ndani ya miaka mitatu ambayo ameendesha matatu, amejenga uhusiano mzuri na abiria kwa kujitolea kwake kubadilisha sekta hiyo.

Taifa Leo ilipompata akiwa kwenye kazi yake, matatu yake ilikuwa imekodishwa na Kwaya ya Kanisa Katoliki la Nyansara kuwasafirisha wanakwaya kutoka Ogembo (Bomachoge Chache) hadi Kegati (Nyaribari Chache) kwa hafla ya maziko.

Mwanamke dereva wa matatu kutoka Kisii, Bi Mercy Ondieki,32, anayeazimia kuibadilisha sekta hiyo kadri ya uwezo wake. Bi Ondieki ni mmoja kati ya madereva wawili wa kike waliosajiliwa chini ya muungano wao mjini Kisii. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Hii si mara ya kwanza kwa kwaya hiyo kutafuta huduma za Bi Ondieki.

Safari ya Bi Ondieki ya kuwa dereva wa matatu ilichochewa na shauku yake kubwa ya kutaka kuleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo kadri anavyoweza.

“Nilipokuwa nikikua, sikuwahi kupenda jinsi baadhi ya wahudumu wa matatu walivyokuwa wakiwatendea wateja wao,” akafichua Bi Ondieki.

Anasema alikasirishwa na baadhi ya madereva na makondakta kutumia lugha chafu kwa abiria.

“Wakati huo sikujua kwamba siku moja ningekuwa katika kazi hii. Lakini sasa nimejipata hapa na tulikubaliana na makanga wangu kwamba tutafanya mambo kwa njia tofauti kwa kuwaonyesha wateja wetu utu kwani hilo ni jambo la msingi kutusaidia kushikilia kazi yetu kwa fahari,” Bi Ondieki akaambia Taifa Leo.

Zake ni sifa teule na za kipekee, ambazo zinamtofautisha na madereva wengine wa matatu.

Bi Cardy Obonyo, mmoja wa wanakwaya waliokuwa wanatumia matatu inayoendeshwa na Bi Ondieki, anasifu viwango vya juu vya nidhamu na kujitolea kwake katika kazi.

“Ni mwanamke anayehitaji kutambuliwa. Nimemfahamu kwa muda mrefu na kila abiria wanapopanda gari lake, wanajihisi salama kwani hawanyanyaswi wala kurushiwa matusi jinsi inavyoshuhudia katika baadhi ya magari ya umma,” Bi Obonyo akasema.

Lakini Bi Ondieki anafichua haijawa rahisi.

Anasimulia jinsi ilivyokuwa vigumu kumshawishi mumewe kwamba angefaulu katika kazi hiyo.

“Mwanzoni hakuunga mkono wazo langu nilipofichua mipango ya kujiunga na sekta hii ya uchukuzi. Kipindi hicho kuna mwajiri aliyekuwa ameniita kufanya kazi kama makanga na hapo mume wangu alipinga vikali. Ilinibidi nimfanye aelewe kwamba nilihitaji kumsaidia maishani ili tuweze kulea familia yetu changa na ndipo akaridhia,” dereva huyo anaeleza.

Pia anataja mapokezi ya chuki aliyopata alipojitosa kwa mara ya kwanza kwenye kazi hivyo, akisema kuwa baadhi ya wafanyakazi wenzake wa kiume walikuwa wakimpa majina ya kila aina.

“Waliniona katika hali mbaya. Wengine wangeniambia kuwa sehemu yangu ilikuwa jikoni lakini baada ya muda nilinyauka haya yote. Sasa wamenikumbatia kama mmoja wao,” Bi Ondieki alisema.

Siku yake huanza saa kumi asubuhi. Anaamka kufanya kazi za nyumbani kwa saa moja. Kufikia saa kumi na moja asubuhi, yuko barabarani tayari kuwasafirisha wateja hadi wanakoenda na kondakta wake Bw Dennis Nyabuto. Wanamaliza shughuli zao saa tatu usiku.

Mwanamke dereva wa matatu kutoka Kisii, Bi Mercy Ondieki,32, anayeazimia kuibadilisha sekta hiyo kadri ya uwezo wake. Bi Ondieki ni mmoja kati ya madereva wawili wa kike waliosajiliwa chini ya muungano wao mjini Kisii. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Bi Ondieki alijifunza kuendesha gari alipokuwa akifanya kazi kama kondakta.

“Dereva niliyekuwa nikifanya naye kazi alinionyesha mambo ya msingi yanayohitajika kuendesha gari. Nilijifunza jinsi ya kusongesha gari ndani ya muda mfupi. Ningependezwa zaidi kuendesha gari wakati tungepeleka gari letu kuliosha kwani hapo nilipata nafasi ya kufanya majaribio,” akasema.

Baadaye alipata leseni na stakabadhi zinazohitajika kwa mtu kuwa dereva wa matatu na mnamo 2021, alipewa kazi na mmiliki mmoja wa matatu ambaye alimkabidhi gari lake.

“Lengo langu ninapofanya kazi kwenye tasnia ni kushikilia taaluma. Tunapaswa kuwatendea abiria kwa heshima wanayostahili kwa sababu sisi si lolote bila wao. Tunahitaji kuwaendesha kwa tahadhari na ni wajibu wetu kama wahudumu wa matatu kuleta mapinduzi katika sekta ya uchukuzi nchini Kenya,” akasema.

Bi Ondieki ni mmoja wa madereva wawili wa kike wa matatu mjini Kisii.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Matatu Kisii Samson Okong’o anawamwagia sifa nyingi.

“Ni madereva wenye uwezo na wenye nidhamu zaidi. Tunapaswa kuwaunga mkono katika kila jambo wanalofanya. Siku zimepita ambapo baadhi ya kazi zilionekana kuwa hifadhi ya jinsia fulani,” Bw Okong’o akasema.