Michezo

Udinese yachelewesha sherehe ya Juve

July 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

JUVENTUS walikosa fursa ya kujitwalia ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu baada ya kuzidiwa maarifa na Udinese katika ushindi wa 2-1 ambao kocha Maurizio Sarri amesema ni wa “kiaibu zaidi” katika historia yake ya ukufunzi.

Juventus ambao wamekuwa mabingwa wa Serie A kwa takriban siku 3,000 ziliopita, wanahitaji kusajili ushindi katika mechi moja pekee kati ya tatu zilizosalia msimu huu ili kunyanyua ufalme wa taji la Serie A kwa mara ya tisa mfululizo.

Beki Matthijs de Ligt aliwaweka Juventus kifua mbele kunako dakika ya 42 kabla ya Ilija Nestorovski kusawazisha mambo katika dakika ya 52. Japo bao hilo la Nestorovski lilitarajiwa kuamsha hamasa ya Juventus, kikosi hicho cha Sarri kilitepetea pakubwa na kuruhusu Seko Fofana kufungia Udinese goli la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili.

“Tumesalia kujilaumu kwa kukosa mpangilio katika kipindi cha pili. Tulitaka sana kuibuka na ushindi katika mechi hii kwa kila namna ambayo ingewezekana. Lakini uzembe ulitugharimu na tukafungwa kiaibu sana sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa,” akasema Sarri ambaye mustakabali wake kambini mwa Juventus kwa sasa unaning’inia pembamba zaidi.

Cristiano Ronaldo wa Juventus kwa sasa amepitwa na  fowadi Ciro Immobile wa Lazio katika vita vya kuwania taji la Mfungaji Bora wa Serie A msimu huu. Immobile alipachika wavuni bao lake la 31 msimu huu katika ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Lazio dhidi ya Cagliari; na hivyo kumzidi Ronaldo kwa goli moja zaidi.

Juventus kwa sasa wanahitaji alama tatu pekee kutokana na michuano mitatu iliyopo mbele yao muhula huu ili kuwapiga kumbo Atalanta, Inter Milan na Lazio ambao ni wapinzani wao wakuu msimu huu.

Katika kile kinachodhihirisha kusenea pakubwa kwa makali ya Juventus, miamba hao wa soka ya Italia wamesajili ushindi katika mechi moja pekee kati ya tano zilizopita. Sarri anatarajia kunyanyua taji la kwanza la ligi katika historia yake ya ukufunzi.

Juventus kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Sampdoria mnamo Julai 26 ila huenda wakawa wameibuka mabingwa wa Serie kufikia wakati wa kupigwa kwa mechi hiyo iwapo Inter Milan watazidiwa maarifa na Genoa nao Lazio waangushwe na Verona katika michuano ya awali ligini.