Michezo

UEFA ina heshima kuliko EPL, Klopp amwambia Guardiola

May 28th, 2019 1 min read

MASHIRIKA NA CECIL ODONGO

MENEJA wa Liverpool Jurgen Klopp amemjibu mwenzake wa Manchester City Pep Guardiola, aliyedai kwamba Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ni ya hadhi kuliko ile ya Klabu Bingwa Barani Ulaya (UEFA).

Guardiola ambaye alishinda EPL kwa mwaka wa pili mfululizo, alijigamba kwamba taji hilo ndilo bora zaidi duniani hasa baada ya kubanduliwa kwenye Uefa na Tottenham Hot Spurs ambao watashiriki fainali dhidi ya Liverpool Jumamosi Julai 1.

Hata hivyo, Klopp ambaye pia anashiriki fainali ya Uefa kwa mwaka wa pili mfululizo, amemjibu mwenzake kwa kumweleza fainali hiyo haisakatwi Uingereza bali uga wa Wanda Metropolitano ambao ni nyumbani kwa Atletico Madrid ya Uhispania.

Kulingana naye hii inaonyesha jinsi fainali hiyo ni ya hadhi mno kuliko EPL anayojivunia Guardiola.

“Pep anajinaki kwamba EPL ni bora kuliko UEFA kwa sababu hajashiriki fainali yake kwa miaka kadhaa sasa. Yeye ni kocha mtajika anayestahili sifa zote anazopewa ila kuhusu hili amenoa kabisa,” akasema Klopp akimjibu Mhispania huyo.

“Ingawa tuliwatoa kijasho chembamba msimu uliokamilika wa 2019/19 katika EPL, walishinda taji hilo kutokana na ubora wa kikosi chao ila wakashindwa kusonga mbele UEFA kwa kutumia kikosi hicho hicho.

“Hii fainali ni ya Bara Ulaya na si Uingereza. Hakuna ubishi kuhusu hilo, hii ni fainali ya mibabe na si Ligi ya Uingereza hata kama ni mara ya tatu tunakutana na Tottenham Hot Spurs,” akaongeza Jurgen Klopp.

Hii ni mara ya tatu kwa Klopp kutinga fainali ya Uefa baada ya kuongoza Borrusia Dortmund kuwakabili mabingwa wa zamani Bayern Munich kwenye fainali ya mwaka wa 2013.