Michezo

UEFA: Kwa kweli soka haina adabu

May 13th, 2019 2 min read

NA JOB MOKAYA

WIKI iliyopita, ulimwengu wa soka ulishuhudia maajabu ya nane ya ulimwengu huku maajabu ya saba yakiwa kule kuvuka kwa mamilioni ya kongoni au nyumbu kutoka mbuga ya MaaSai Mara nchini Kenya kuelekea mbuga ya Serengeti, Tanzania.

Timu ya Liverpool kutoka Uingereza iliishinda miamba wa soka ya Uhispania, Barcelona kwa mabao manne bila jibu lolote na hivyo kufuzu kwa fainali ya Kombe la Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) msimu huu. Mpambano huo ulipigiwa uwanjani Anfield kule Uingereza.

Awali, Barcelona ilikuwa imeishinda Liverpool kwa magoli matatu bila kurejeshewa chochote katika awamu ya kwanza iliyopigwa majuma mawili yaliyopita katika uchanjaa wa Camp Nou, Uhispania.

Mabao mawili ya Messi na jingine moja la Luis Suarez yalitosha kuzamisha Liverpool ndani ya kilindi cha tope mbele ya mashabiki wa Barcelona.

Katika awamu ya marudiano, Liverpool ilihitaji kufunga mabao manne ili kufuzu, jambo ambalo si rahisi haswa unapocheza dhidi ya Barcelona, tena Barcelona inayojivunia huduma za mchezaji bora zaidi duniani, Lionel Messi kutoka Argentina, Amerika ya Kusini.

Kwa Liverpool, hali yao ilizidi kuwa ngumu zaidi pale ambapo wachezaji wawili muhimu ambao wangefunga mabao hayo yaliyohitajika sana walikosa kucheza. Mohamed Salah alipata jeraha baya katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Newcastle United, naye Robert Firmino raia wa Brazil akawa ameumia mapema kidogo.

Sadio Mane alijipata peke yake pale mbele akiwa na watu asiowafahamu vyema – fowadi wa Ubelgiji mwenye asili ya Kenya, Divock Origi (mwanawe Mike Okoth, yule mshambulizi wa zamani wa Harambee Stars) pamoja na Xhedarn Shaqiri.

Barcelona nao kwa kujua hali ilivyokuwa, walitua Liverpool wakijishaua sana na kutawaliwa na matumaini tele. Matumaini ambayo hayakutimia pale ambapo Origi alicheka na wavu mara mbili naye Mholanzi Georginio Wijnaldum akafunga mabao mawili na kuzamisha kabisa chombo cha Barcelona ugani Anfield.

Wachezaji wa Barcelona hawakuamini kwamba wangefungwa mabao manne bila jawabu hata baada ya wachezaji wa timu hiyo kupata mapumziko ya kutosha. Hata yule mshambuliaji wao hatari anayeitwa Messi alikataa kabisa kupanda basi la timu hiyo na badala yake kuamua kupiga milundi kuelekea hotelini.

Muujiza mwingine wa nane ulifanyika huko Uholanzi wakati Tottenham ilitoka nyuma kwa mabao matatu na kuishinda Ajax Amsterdam kwa mabao matatu kwa mawili na hivyo kutinga fainali. Tottenham ilikuwa imeshindwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Wembley kwa bao moja kwa bila jibu.

Baada ya kipenga cha mapumziko kupulizwa, tayari magoli mawili yalikuwa yameingia katika mlango wa Tottenham. Hivyo, timu hii ya kocha Mauricio Pochettino ilihitaji muujiza wa kufunga mabao matatu na kuzuia bao lolote kuingia golini mwao ili ifuzu.

Amini usiamini, muujiza huo ulitendeka. Tottenham ambayo pia haikuwa na mchezaji wake wa kutegemewa, Harry Kane ilileta mchezaji asiyejulikana sana kwa wapinzani – Lucas Moura raia wa Brazil

Ili kujaza pengo lililoachwa wazi na Kane. Na ni huyo Moura aliyefanya mambo kwa kutia tunduni mabao matatu katika kipindi cha lala-salama; na hilo la tatu likaingia katika dakika ya mwisho ya mchezo, la sivyo

Tottenham ingeelekezwa nyumbani na limbukeni Ajax.

Matukio haya mawili yanadhihirisha kwamba soka haina adabu. Soka ya leo si kama soka ya zamani. Zamani kila mmoja alijua kwamba Brasil ingelishinda timu yoyote kwa urahisi katika kipute cha kuwania Kombe la Dunia. Soka haina huruma.

Brazil ilipigwa magoli saba kwa moja na Ujerumani katika fainali za Kombe la dunia kuko huko Brazil mnamo 2014. Hakika, soka haina adabu!