Michezo

UEFA: Liverpool, Barcelona, Inter, Gala, Dortmund na Atletico zavuna ushindi

September 19th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MIBABE wa soka ya Uingereza Liverpool, Jumanne usiku walidhihirisha weledi wao katika anga za kuwania Kombe la Klabu Bingwa Barani Uropa walipovuna ushindi wa 3-2 dhidi ya PSG ya Ufaransa katika mechi kali iliyosakatwa ugani Anfield.

The Reds walichukua uongozi wa mchuano huo kupitia straika Daniel Sturridge katika dakika ya 30 ya mechi hiyo.   Katika dakika ya 36 nyota iliendelea kung’aa kwa kikosi cha The Reds wakati difenda Gini Wijnaldum alipoangushwa katika eneo  hatari na vijana wa kocha  Jurgen Klopp kupokezwa penalti iliyofungwa kiustadi na James Milner.

Hata hivyo PSG hawakukata tamaa na wakatunikiwa bao safi dakika 5 baada ya kipindi cha pili kuanza wakati beki wa kulia Thomas Meunier alipofuma wavuni bao zuri na mambo yakawa 2-1.

Katika dakika ya 53 mshambulizi wa Liverpool Mohamed Salah alifungua bao alilodhani lingewapunguzia shinikizo ila likafutiliwa mbali kwa kuwa aligongana na kipa wa PSG Alphonse Areola.

Hata hivyo pasi mbovu ya Salah iliwaponza Liverpool kisha mchezaji nyota Neymar na Van Dijk kuonana vizuri na kumpokeza Kyle Mbappe pasi safi iliyowazalishia PSG goli la pili na kufanya mambo kuwa mabao 2-2.

Hata hivyo, Roberto Firmino aliibuka mwokozi wa Liverpool kwa kutia msumari moto kwenye kidonda cha PSG dakika ya 92 kwa kufunga bao na kuhakikishia timu yake alama zote tatu.

Wawikilishi wengine kutoka Uingereza Tottenham Hotspur waliangukia pua kwa kichapo cha 2-1 mikononi mwa Inter Milan ya Italia huku  mabingwa wa zamani Barcelona wakiangusha PSV ya Uholanzi 4-0 mtanange ambao Lionel Messi alifunga mabao matatu.

Mabingwa wa mwaka 2017/2018  ligi ya Uropa Atletico Madrid waliicharaza Monaco 2-1 ugenini, Schalke 04 ikaagana  sare ya 1-1 na FC Porto  kisha Dortmund ikailaza Club Brugge 1-0.

Napoli na Red Star Belgrade zilitoka sare tasa nao Galatasary ya Uturuki ikaiadhibu Lokomotiv Moscow mabao 3-0.