HabariMichezo

UEFA: Liverpool waichinja Barcelona na kutinga fainali

May 8th, 2019 2 min read

NA FAUSTINE NGILA

LIVERPOOL, UINGEREZA

NI HISTORIA! Vijana wa kocha Jurgen Klopp wametinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya Jumanne usiku baada ya kuitia adabu Barcelona 4-0 ugani Anfield katika mechi ya marudiano.

Makeke ya mashabiki yalionekana kuisaidia Liverpool kuizima Barcelona, ambayo iliwapiga 3-0 uwanjani Camp Nou na kuchochea wachanganuzi wengi wa soka kuanza kuipuuza Liverpool, na kusisitiza haikuwa na nafasi ya kufika fainali.

Ni mara ya kwanza tangu mwaka 1986  – wakati Barcelona iliiondoa Gothenburg kwenye pambano hili – ambapo timu imetoka nyuma 3-0 na kushinda mechi ya pili ya nusu fainali.

Straika mzaliwa wa Kenya Divock Origi alikuwa wa kwanza kuonja bao dhidi ya kipa Ter Stegen alipotia kimiani gozi katika dakika ya saba. Lakini kiungo Georginio Wijnaldum alipochukua nafasi ya Robertson, maji yalizidia Barca unga alipowapiga makombora mawili katika muda wa dakika mbili katika kipindi cha pili.

Aidha, matokeo yakiwa 3-3 kijumla, ilibidi beki wa kupanda na kushuka Trent Alexander-Arnold kucheza na akili za madifenda wa Barcelona na kupiga mpira wa kona kwa kasi isiyotarajiwa, ambapo Origi alifunga kazi kwa kucheka na wavu na matokeo ya 4-3 yakawafikisha fainaali ‘miamba wa soka duniani’.

Barcelona waliteswa, wakahangaishwa, wakaduwazwa, wakadhalilishwa kisha wakasagwa na kumumunywa kama pipi huku nahodha wao Lionel Messi akitazama tu, asijue la kufanya ila kujutia kukosa kuilima Liverpool 5-0 ugani Camp Nou.

Kipenga cha mwisho kilililetea jiji zima la Liverpool, majirani Everton, na Uingereza kwa jumla nderemo na vifijo na kuondoa imani ya muda mrefu kuwa timu za Uhispania haziwezi kuzidiwa maarifa na timu za Uingereza kwenye UEFA.

Ikumbukwe Liverpool wanatambulika kwa kutoka nyumba katika mapambano muhimu, hasa kwenye fainali ya 2005 ambapo ilitoka nyumba 3-0 kipindi cha kwanza dhidi ya AC Milan na kushinda taji hilo kwa mara ya tano.

Hii ni mara ya pili kwa Barcelona kuondolewa kwenye kipute hiki ndani ya miaka miwili. Msimu uliopita, timu ya Roma kutoka Italia ilikubali kichapo cha 4-1 uwanjani Camp Nou, lakini ikaipa Barcelona kipigo cha 3-0 katika mechi ya marudiano na kutinga nusu fainali kwa jumla ya mabao 4-4, kutokana na bao la ugenini.

Kwa sasa, mafundi wa soka Liverpool wanatazamia kushinda kombe hili kwa mara ya sita hapo Juni mosi jijini Madrid, Uhispania, watakapomenyana na ama Ajax au Tottenham.