Michezo

UEFA: Mipango ipo kukamilisha Champions League na Europa League Agosti 2020

May 17th, 2020 2 min read

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

RAIS wa soka ya bara Ulaya (Uefa), Aleksander Cerefin, amesema kwamba shirikisho hilo lina “mipango madhubuti” ya kukamilisha kampeni zote za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Europa League kufikia mwisho wa Agosti, 2020.

Robo-fainali na nusu-fainali za vipute hivyo zitahusisha michuano ya mikondo miwili; yaani mechi kuchezwa na kila kikosi nyumbani na ugenini.

“Mambo yalivyo, nina hakika kwamba tutakamilisha kampeni za soka ya Uefa msimu huu,” akasema Cerefin.

Kinara huyo amesisitiza kwamba michuano yote iliyosalia itatandazwa ndani ya viwanja vitupu na ni matumaini yake kwamba ligi kuu nyingi za bara Ulaya zitakamilisha kampeni za muhula huu.

Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) inayotazamiwa kuanza upya mnamo Juni 12 imesalia na raundi tisa zaidi muhula huu huku Paris Saint-Germain (PSG) wakitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa baada ya msimu huu wa 2019-20 kufutiliwa mbali.

Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ilirejelewa Mei 16, 2020, na ni matumaini kwamba vipute vya Uhispania (La Liga) na Italia (Serie A) vitaanza upya mnamo Juni 13 baada ya wanasoka wote wa klabu za ligi hizo kurejea kambini na kuanza mazoezi.

Kwa mujibu wa Cerefin, klabu zote ambazo ligi zao hazitatamatika rasmi muhula huu zitalazimika kushiriki mchujo ili kufuzu kwa mashindano ya Uefa muhula ujao.

“Hiyo ndiyo itakuwa fomula ya pekee ya kujikatia tiketi za kunogesha vipute vya UEFA na Europa League muhula ujao,” akasema.

Mashindano ya Euro 2020 yaliyokuwa yaandaliwe kuanzia Juni 12 – Julai 12, 2020 sasa yameahirishwa hadi Juni 11 – Julai 11, 2021 baada ya mwafaka wa kuyasogeza mbele kufikiwa mnamo Machi 2020.

Nusu-fainali na fainali ya kipute hicho cha Euro zitapigiwa uwanjani Wembley, London, Uingereza huku michuano ya hatua nyinginezo ikisakatiwa katika miji ya Amsterdam, Baku, Bilbao, Bucharest, Budapest, Copenhagen, Dublin, Glasgow, Munich, Rome na St Petersburg.

Kwa mujibu wa Cerefin, maazimio yao ni kufanikisha maandalizi ya Euro 2021 katika miji mitatu ya awali na Uefa kwa sasa inajadiliana na wasimamizi miji mingine tisa tofauti itakayokuwa wenyeji wa baadhi ya michuano.

“Sioni uwezekano wa kampeni za Euro kufanyika katika miji mitatu pekee. Tunazidi kushauriana na miji mingine tisa ili tuwe na jumla ya 12 japo 10, tisa au hata minane bado itakuwa sawa,” akaongeza.