UEFA Robo Fainali: Bayern vs PSG, Real Madrid vs Liverpool

UEFA Robo Fainali: Bayern vs PSG, Real Madrid vs Liverpool

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL watakutana na Real Madrid kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Manchester City wametiwa katika zizi moja na Borussia Dortmund huku Chelsea wakipangwa pamoja na FC Porto. Mabingwa watetezi Bayern Munich watakutana na Paris Saint-Germain (PSG), timu ambayo waliipiga kwenye fainali ya UEFA mnamo 2019-20 jijini Lisbon, Ureno.

Katika nusu-fainali, mshindi kati ya Real na Liverpool atakutana na mshindi wa gozi kati ya Porto na Chelsea huku Man-City au Dortmund wakikutana na mshindi kati ya Bayern na PSG.

Mechi za mikondo miwili ya robo-fainali itasakatwa kati ya Aprili 6-7 na Aprili 13-14, 2021.

Michuano ya mkondo wa kwanza wa nusu-fainali itatandazwa kati ya Aprili 27-28 huku marudiano yakiandaliwa kati ya Mei 4-5, 2021.

Liverpool na Real waliwahi kukutana kwenye fainali ya UEFA mnamo 2018 na miamba hao wa Uhispania wakashinda 3-1 na hivyo kutia kapuni taji lao la 13 kwenye historia ya kivumbi hicho.

Timu hizo mbili zimewahi kukutana mara sita kwenye soka ya UEFA, kila mmoja akishinda mara tatu, ukiwemo ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Liverpool katika fainali ya 1981.

Mara ya mwisho kwa vikosi hivyo kukutana kwenye hatua ya mwondoano wa UEFA ni 2009 walipovaana katika hatua ya 16-bora. Liverpool waliibuka na ushindi wa jumla ya mabao 5-0 na kudengua Real.

Man-City ambao kwa sasa wanaongoza jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamewahi kukutana na Dortmund mara moja pekee, katika hatua ya makundi ya UEFA mnamo 2012. Wakati huo, Man-City walilazimishiwa sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza uwanjani Etihad kabla ya kupigwa 1-0 kwenye marudiano yaliyoandaliwa ugani Signal Iduna Park, Ujerumani.

Man-City wanaowania kombe la UEFA kwa mara ya kwanza, wanafukuzia jumla ya mataji manne msimu huu. Huenda wakakutana na fowadi chipukizi raia wa Uingereza, Jadon Sancho, aliyeagana nao mnamo 2017 na kuyoyomea Dortmund.

Fowadi matata raia wa Norway, Erling Braut Haaland ambaye ni mtoto wa kiungo wa zamani wa Man-City, Alf-Inge Haaland, pia anachezea Dortmund na amefungia kikosi hicho jumla ya mabao 20 kutokana na mechi 14 zilizopita za UEFA.

Kufikia sasa, Dortmund wanashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga). Walimfuta kazi kocha Lucien Favre mnamo Disemba 2020 na kumpa mikoba mkufunzi mshikilizi Edin Terzic.

Chelsea wamewahi kukutana na Porto mara nane, wakashinda mara tano na kupoteza mara mbili. Mabingwa hao wa zamani wa EPL waliwalaza Porto ambao ni miamba wa soka kutoka Ureno kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo 2007.

Kocha Thomas Tuchel ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Chelsea, aliwaongoza PSG kutinga fainali ya UEFA mnamo 2019-20 na wakapokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Bayern. Bao hilo la pekee lilifumwa wavuni na kiungo mvamizi raia wa Ufaransa, Kingsley Coman na Bayern wakashinda taji la UEFA kwa mara ya sita.

Tuchel aliagana rasmi na PSG mwishoni mwa Disemba 2020 na akapokezwa mikoba ambayo Chelsea walimpokonya kocha Frank Lampard mnamo Januari 2021.

DROO YA ROBO-FAINALI ZA UEFA 2020-21:

Manchester City na Borussia Dortmund

Porto na Chelsea

Bayern Munich na Paris St Germain

Real Madrid na Liverpool

DROO YA NUSU-FAINALI ZA UEFA 2020-21:

Bayern au PSG na Man-City au Dortmund

Real au Liverpool na Porto au Chelsea

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kilimo bila kemikali kinalipa, Sylvia asimulia

Europa: Man-Utd vs Granada, Arsenal vs Slavia Prague