Michezo

UEFA: Shabiki wa Liverpool afariki akisherehekea bao la Origi

May 9th, 2019 1 min read

MASHIRIKA NA CHARLES WASONGA

SHABIKI wa Liverpool alifariki juzi alipokuwa akisherehekea bao la nne la timu hiyo dhidi ya timu ya FC Barcelona katika mechi yanusu fainali ya mchuano wa Klabu Bingwa (UEFA) barani Uropa.

Goli hilo lilitiwa kiamiani na mshambulizi matata wa Liverpool Divock Origi baada ya kuunganisha kona iliyochanjwa na beki Trent Alexander-Arnold.

Kulingana na tovuti ya spoti ya Ghanaweb.com, Hebert Dansp Atiko, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho anayesomea uhandisi katika Chuo cha Kiufundi cha Akwatia (Akwita Technical School) alianguka vibaya sakafuni bila ufahamu timu hiyo ya Uingereza ilipofunga goli hilo na kuwaacha vijana wa Barcelona hoi.

Goli hilo liliyeyusha kabisa matumaini ya mabingwa hao wa ligi ya kuu ya Uhispania kufika fainali ya mchuano huo.

Msimamizi wa taasisi hiyo, Michael Okyere kwenye mahojiano na wanahabari alisema marafiki wa marehemu walijaribu kummwagia maji baridi kumfufua lakini juhudi zao ziliambulia pakavu.

Hapo ndipo wakamkimbiza katika hospitali ya St Dominic, mjini Akwatia, lakini madaktari wakathibitisha kuwa alikuwa amakata roho.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa nne, ambaye ilisemekana alikuwa akifanya mtihani wake wa mwisho, ana umri wa miaka 29.

Katika mkondo wa kwanza wa nusu fainali hiyo Barcelona ilicharaza Liverpool mabao 3-0.

Lakini juzi waliwashtua miamba hao wa Uhispania kwa kuwazima magoli 4-0 na kujikatia tiketi ya fainali ambapo wakagarazana na timu ya Tottenham Hotspurs.

Mnamo Jumatano usiku Spurs iliandikisha historia kwa kuchapa makinda wa Ajax magoli 3-2 na kufuzu kwa fainali itakayogaragazwa mnamo Juni mosi jijini Madrid, Uhispania.

Katika fainali hiyo Wakenya watajigawa kuwili kushabikia Tottenham ambako Victor Wanyama anasakatia na Liverpool ambapo Divock Origi (mwanawe mchezaji wa zamani wa Harambee Star Mike Okoth) anawajibikia.