Michezo

UEFA SUPER CUP: Bayern watoka nyuma na kulaza Sevilla

September 25th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

BAYERN Munich walihitaji bao la Martinez Aguinaga katika muda wa ziada kuwapiga Sevilla 2-1 katika gozi la kuwania taji la Uefa Super Cup lililosakatiwa jijini Budapest, Bulgaria mnamo Septemba 24, 2020.

Mchuano huo ulihudhuriwa na mashabiki 15,180 katika uwanja wa Puskas Arena ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 67,000.

Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza ya bara Ulaya kushuhudia mashabiki wakihudhuria ugani tangu kulipuka kwa janga la corona mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020.

Ingawa Bayern walipigiwa upatu wa kuwaangusha Sevilla kirahisi, vijana wa kocha Hansi Flick walitolewa jasho na wakaonekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara.

Chini ya kocha Julen Lopetegui, Sevilla walijiweka kifua mbele kunako dakika ya 13 kupitia penalti iliyochanjwa na Lucas Ocampo.

Penalti hiyo ilichangiwa na tukio la kiungo wa zamani wa Barcelona, Ivan Rakitic, kuchezewa visivyo na beki David Alaba ndani ya kijisanduku.

Hata hivyo, Bayern walisawazisha mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia kwa kiungo mvamizi Leon Goretzka aliyeshirikiana vilivyo na fowadi matata raia wa Poland, Robert Lewandowski.

Vikosi vyote vilianza kipindi cha pili kwa matao ya juu huku kila upande ukiwa tishio langoni pa mpinzani.

Mabeki wa Sevilla walisalia imara licha ya presha iliyotolewa na Lewandowski na sajili mpya wa Bayern, Leroy Sane aliyeagana na Manchester City mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.

Hata hivyo, Sevilla nao walipata fursa nzuri za kuwafunga Bayern ila kipa Manuel Neuer akajitahidi zaidi na kumnyima Youssef En-Nesyri nafasi mbili za wazi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Bayern ambao walipoteza mechi kwa mara ya mwisho mnamo Disemba 2019, walipata ushindi wao kupitia kwa Martinez kunako dakika ya 104.

Nyota huyo raia wa Uhispania alikamilisha kwa kichwa krosi safi ya Alaba na kumwacha hoi kipa Yassine Bounou.

Bayern ambao ni wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) waliwacha nje baadhi ya wanasoka mahiri kama vile Alphonso Davies katika mechi hiyo.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na German Cup mnamo 2019-20, walionekana walegevu na wachovu kwa wakati fulani licha ya kuanza vyema kampeni zao za Bundesliga kwa ushindi mnono wa 8-0 dhidi ya Schalke 04 mnamo Septemba 18, 2020.

Ingawa hivyo, Flick amesisitiza kwamba vijana wake wana kiu ya kuhifadhi pia taji la UEFA walilojitwalia mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuwapiga Paris Saint-Germain (PSG) 1-0 jijini Lisbon, Ureno.

Huku ushindi wa Bayern dhidi ya Sevilla ukiendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 32 mfululizo, rekodi ya Sevilla ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 21 mfululizo ilifikia kikomo cha ghafla.