Michezo

UEFA yampiga marufuku straika wa Ukraine kwa kutumia pufya

June 6th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Ukraine, Artem Biesiedin, 24, amepigwa marufuku ya mwaka mmoja na Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli (pufya).

Vipimo vilivyofanyiwa damu ya nyota huyo wa kikosi cha Dynamo Kiev vilionyesha kwamba ilikuwa na chembechembe nyingi za dawa za kuongeza nguvu mwilini.

Inadaiwa kwamba mwanasoka huyo alitumia dawa hizo wakati alipowaongoza waajiri wake Kiev kupepetana na Malmo katika mojawapo ya mechi za makundi katika kipute cha Europa League mnamo Novemba 2019.

Marufuku ya Biesiedin yanaanza kutelekezwa Disemba 19, 2019 wakati ambapo vipimo vya damu yake vilifanywa na hadi kufikia sasa, hajakata rufaa dhidi ya maamuzi hayo.

Sogora huyo ambaye anajivunia kufungia Ukraine mabao mawili katika soka ya kimataifa atakuwa huru kunogesha kivumbi cha Euro 2021 baada ya mashindano hayo yatakayoandaliwa katika mataifa 12 tofauti ya bara Ulaya kuahirishwa kutokana na janga la corona.

Mwaka jana, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilitoa wito wa kubadili njia za mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwenye mchezo huo.

Ikiwa imepita miezi minne tu baada Shirika la Kimataifa la kupambana na dawa za kusisimua misuli (WADA) kufanya mkutano jijini Johannesburg, Afrika Kusini, FIFA pia ilitarajiwa kuandaa mkutano wao kwenye makao makuu ya shirikisho hilo jijini Zurich, Uswizi mnamo Aprili 2020 kabla ya janga la corona kuwa kiini cha kuahirishwa kwa kikao hicho.

Mkutano huo ulitarajiwa kutoa jukwaa la kujadiliwa kwa baadhi ya mbinu maridhawa zaidi za kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli miongoni mwa wanasoka na adhabu kwa makosa ya kutumia pufya.