Michezo

UEFA yatoza PSG faini ya Sh3.7 milioni kwa kujikokota kurudi uwanjani kipindi cha pili mechi dhidi ya Atalanta

August 15th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) wametozwa faini ya Sh3.7 milioni kwa hatia ya kutorejea uwanjani kwa wakati uliostahili baada ya mapumziko ya kipindi cha kwanza walipokuwa wakivaana na Atalanta kwenye robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

PSG waliibuka washindi wa mechi hiyo iliyochezewa jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 12, 2020 na hivyo kujikatia tiketi ya kuvaana na RB Leipzig ya Ujerumani kwenye hatua ya nusu-fainali kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25. Nusu-fainali hiyo itapigiwa jijini Lisbon mnamo Agosti 18, 2020.

Leipzig waliwabandua Atletico Madrid ya Uhispania kwenye hatua ya nane-bora kwa mabao 2-1, hii ikiwa idadi sawa ya mabao ambayo PSG walifunga dhidi ya Atalanta ya Italia.

Kocha Thomas Tuchel wa PSG pia ameonywa vikali na Uefa kwa kutowajibika ipasavyo na kuchangia kukawia kuanzishwa kwa kipindi cha pili wakati wa mechi dhidi Atalanta. Mechi hiyo ilicheleweshwa kwa dakika saba.

Uefa inawaadhibu PSG siku moja baada ya kuwatoza Sevilla faini ya Sh1.2 milioni kwa kuchelewa kufika uwanjani wakati wa mechi ya robo-fainali ya Europa League iliyowakutanisha na Wolves mnamo Agosti 11, 2020.

Sevilla ambao ni mabingwa mara tano wa kipute cha Europa League, waliwapokeza Wolves kichapo cha 1-0 katika mechi hiyo iliyowakatia tiketi ya kupepetana na Manchester United kwenye nusu-fainali itakayoandaliwa mjini Dusseldorf, Ujerumani mnamo Agosti 16, 2020.