Ufaransa kukutana na Uhispania kwenye fainali ya UEFA Nations League baada ya kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha Ubelgiji

Ufaransa kukutana na Uhispania kwenye fainali ya UEFA Nations League baada ya kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha Ubelgiji

Na MASHIRIKA

THEO Hernandez alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili na kusaidia mabingwa wa dunia Ufaransa kutoka chini kwa magoli 2-0 na kuwatandika Ubelgiji 3-2 katika ushindi uliowakatia tiketi ya kuonana na Uhispania kwenye fainali ya UEFA Nations League.

Chini ya kocha Didier Deschamps, masogora wa Ufaransa walionekana kudenguliwa kwenye kipute hicho baada ya kufungwa mabao mawili ya haraka chini ya dakika nne za kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, kikosi hicho kilichoshinda Croatia 4-2 na kunyanyua Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi kilitegemea maarifa ya Hernandez wa AC Milan kujizolea ushindi muhimu sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa uwanjani Alliaz Stadium jijini Turin, Italia.

Ubelgiji wanaonolewa na kocha Roberto Martinez waliwekwa uongozini na Yannick Carrasco aliyemwacha hoi kipa Hugo Lloris wa Ufaransa katika dakika ya 37.

Dakika nne baadaye, Ubelgiji wanaoorodheshwa wa kwanza kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), walifungiwa bao la pili na Romelu Lukaku aliyekamilisha krosi safi kutoka kwa Kevin De Bruyne.

Hata hivyo, Karim Benzema aliwarejesha Ufaransa mchezoni kunako dakika ya 60 baada ya kushirikiana vilivyo na Kylian Mbappe aliyesawazisha mambo kupitia penalti katika dakika ya 69. Penalti hiyo ilitokana tukio la Antoine Griezmann kuchezewa visivyo na Youri Tielemans.

Lukaku alidhani alikuwa amefungia Ubelgiji bao la ushindi kunako dakika ya 87 baada ya kushirikiana na Carrasco ila goli lake likafutiliwa mbali na teknolojia na VAR iliyobaini kwamba alikuwa ameotea.

Kabla ya Hernandez kufunga bao la ushindi, Paul Pogba wa Ufaransa alishuhudia kombora lake kutoka hatua ya 30 likigonga mwamba wa lango la Ubelgiji.

Fainali ya Nations League mwaka huu imepangiwa kufanyika Jumapili ya Oktoba 10, 2021 uwanjani San Siro baada ya mechi ya kutafuta mshindi nambari tatu na nne kati ya Ubelgiji na Italia ambao ni mabingwa wa Euro kundaliwa jijini Turin.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jubilee kuachia kila raia deni la Sh180,000

Hofu ya Pwani kususia kura za 2022 yatanda