Michezo

Ufaransa, Ujerumani kutoana jasho kirafiki

March 22nd, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

LYON, Ufaransa

MIAMBA Ufaransa na Ujerumani watafufua uhasama ugani Groupama kwenye mechi ya kupimana nguvu ambayo wenyeji wanapigiwa upatu kufaulu kulipiza kisasi.

Aidha, Poland, Wales, Ugiriki, Georgia, Iceland na Ukraine waliweka hai matumaini kufuzu kushiriki Kombe la Ulaya (Euro2024) baada ya kuzoa ushindi katika nusu-fainali za muondoano Alhamisi.

Les Bleus walipoteza 2-1 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Die Mannschaft kupitia mabao ya Thomas Muller na Leroy Sane walipokutana mara ya mwisho Septemba 2023 ugani Signal Iduna Park, Dortmund wakati Antoine Griezmann alifunga bao la kufutia machozi.

Hata hivyo, vijana wa kocha Didier Deschamps wako katika orodha ya timu zinazopigiwa upatu kushinda Kombe la Ulaya (Euro) 2024 nchini Ujerumani na watatumai kutumia mtihani wa Jumamosi kupima uthabiti ama ulegevu wao.

Mshambulizi matata Kylian Mbappe ni mmoja watakaotegemewa na Deschamps katika mchuano huo.

Ni mchuano ambao pia Wajerumani watapima utayari wao wakilenga kuepuka aibu kwenye Euro 2024 baada ya kubanduliwa makundini wakati wa Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Griezmann atakosa mechi ya Ufaransa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka saba baada ya nyota huyo wa Atletico Madrid kujiondoa kikosini kwa sababu ya jeraha la kifundo. Kuna hofu pia kuhusu kipa Mike Maignan.

Ujerumani, ambayo kuanzia mwaka 2027 itavalia jezi kutoka Nike baada ya kusaini kandarasi na kampuni hiyo ya Amerika hapo Alhamisi baada ya kuwa na Adidas tangu 1950, itakosa huduma za kipa Manuel Neuer. Anauguza jeraha.

Kocha Julian Nagelsmann, ambaye anaaminika kumezewa mate na Liverpool FC, anakaribisha Toni Kroos, 34, kikosini. Kroos hajachezea Ujerumani tangu atangaze baada ya Euro2020 kuwa amestaafu kuchezea timu ya taifa. Alithibitisha kurejea kikosini hapo Alhamisi.

Katika kampeni za kunyakua tiketi tatu za mwisho za Euro2024, Ugiriki walilipua Kazakhstan 5-0 jijini Athens, Poland wakalima Estonia 5-1 (Warsaw), Wales wakapepeta 4-1 (Cardiff) nao Iceland wakanyamazisha wenyeji Israel 4-1 (Hungary). Georgia walichapa Luxembourg 2-0 (Tblisi) nao Ukraine wakalima wenyeji Bosnia & Hezegovina 2-1 (Zenica).

Mshindi kati ya Wales na Poland pamoja na Ukraine na Iceland, na Georgia na Ugiriki wataungana na timu 21 zilizofuzu wakati wa mechi za makundi kushiriki Euro2o24 mnamo Juni 14 hadi Julai 14.

Katika baadhi ya mechi za kirafiki zilizosakatwa Alhamisi, Ureno ilibomowa Uswidi 5-2, Italia ikapepeta Venezuela 2-1, Urusi ikachabanga Serbia 4-0, Belarus ikasalimu amru ya Montenegro 2-0 Ethiopia ikalimwa 2-1 na Lesotho nayo Guinea ikalipua Vanuatu 6-0.