Ufaransa waponea kushushwa ngazi kwenye Uefa Nations League licha ya kutandikwa na Denmark ugenini

Ufaransa waponea kushushwa ngazi kwenye Uefa Nations League licha ya kutandikwa na Denmark ugenini

Na MASHIRIKA

MABINGWA wa dunia, Ufaransa, waliponea chupuchupu kuteremshwa ngazi kutoka makundi ya vikosi vya haiba kubwa kwenye Uefa Nations League licha ya Denmark kuwapokeza kichapo cha 2-0 mnamo Jumapili.

Ufaransa walikamilisha kampeni zao za Kundi A1 katika nafasi ya tatu kwa alama tano, moja zaidi kuliko Austria walioshushwa daraja baada ya Croatia kuwapepeta 3-1. Denmark ni wa pili kwa pointi 12, moja nyuma ya Croatia wanaoselelea kileleni.

Licha ya ushindi, Denmark walikosa kufuzu kwa fainali za Nations League mwakani. Walihitajika kushinda na kutumainia kwamba Croatia wangeangushwa na Austria kwenye pambano jingine la Kundi A1 ili kufuzu kwa fainali za Juni 14-18, 2023.

Kasper Dolberg na Andreas Skov Olsen walifungia wenyeji Denmark mabao yao katika kipindi cha pili cha mchuano huo uliosakatiwa jijini Copenhagen.

Ufaransa waliokomoa Uhispania 2-1 katika fainali ya Nations League 2021, walikomesha rekodi duni ya kutoshinda mechi nne mfululizo mnamo Alhamisi iliyopita kwa kutandika Austria 2-0 jijini Paris na kujitoa kwenye mkiani wa kundi.

Ingawa Kylian Mbappe wa Ufaransa alimwajibisha sana kipa Kasper Schmeichel ugani Parken, Denmark ndio walitamalaki mchezo wa Jumapili ulioshuhudia kiungo mpya wa Manchester United, Christian Eriksen, akishirikiana vilivyo na Skov Olsen na Dolberg katika safu ya mbele.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Italia wakomoa Hungary jijini Budapest katika Uefa Nations...

Wakulima walilia serikali gharama ikizidi kupanda

T L