Kimataifa

Ufasaha wa lugha waokoa vijana waliopatikana na bangi

January 7th, 2019 2 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

MAHAKAMA moja nchini Uingereza ilishangaza wengi ilipowasamehewanafunzi wawili walioshtakiwa kwa kupatikana na bangi, na kukosa kuwsukuma jela, ikisema walitumia lugha mufti ajabu.

Jaji David Hale ambaye aliamua kesi ya Luke Rance, 19 na Brandon Kerrison, 21 aliridhishwa na usanifu wa wanafunzi hao, akiamua kuwafunga kifungo cha nje badala ya jela, kutokana na usanifu wao.

Mahakama hiyo ilisema kuwa lugha ya washukiwa hao ilikuwa ya hali ya juu, ikilinganishwa na ile ya walanguzi wa dawa za kulevya wa kila siku.

Rance alidaiwa kununua bangi kiwango kikubwa na kumuuzia Kerrison ambaye alikuwa akiuzia watu eneo la Gower, Swansea, mahakama ilielezwa.

Wawili hao walikamatwa Desemba 17, 2017 wakati maafisa wa polisi waliokuwa wakipiga doria kwa miguu walipigwa na harufu walipokuwa wakipita karibu na maktaba, kijiji cha Pennard.

Rance alipatikana na magunia saba ya bangi na kiwango kidogo cha Cocaine. Kerrison naye alikamatwa na magunia mawili ya bangi ya matibabu.

Vyumba vyao vya kulala vilipopigwa msako na polisi vilevile, bangi ya zaidi ya Sh1.2milioni ilipatikana katika chumba cha Rance.

Polisi aidha walikagua simu za mkononi za wawili hao ambapo katika jumbe fupi zilizopatikana, Jaji Hale alibaini kuwa matumizi ya lugha sanifu yalikuwa ya kiwango cha juu, pamoja na sarufi ikilinganishwa na lugha inayotumiwa na walanguzi kikawaida.

Ujumbe mmoja kutoka kwa simu ya Kerrison kwa zaidi ya nambari moja ulisema; “Fleva za kiwazimu kuanzia saa nne usiku wa leo – nifahamishwe kwa habari zaidi.”

Korti ilielezwa kuwa Kerrison majuzi alikamilisha kozi ya ujenzi, ilhali Rance mbeleni aliwahi kuhusika katika maigizo, na kuwa anaelekea kuanza masomo ya shahada.

Wote walikiri kosa la kupatikana na bangi kwa lengo la kusambaza, huku Rance akizidi kukiri kupatikana na Cocaine. Wote hawajawahi kufungwa mbeleni.

Jaji huyo alisema “Bangi inawezakuwa jaribio ambalo mnalipata kuwa la raha” lakini akaonya wawili hao kuhusu hatari zilizopo.

Jaji huyo alisema hakutaka kuwaharibia maisha vijana hao kwa kuwafunga jela, lakini akawafunga wote miezi 12 kifungo cha jamii, kwa kufanya kazi saa 100 bila malipo.