Makala

UFISADI: Afisa mteule EACC afichua alinolewa katika FBI na CIA, Amerika

December 14th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

AFISA MPYA aliyeteuliwa kwa wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak ameahidi kurejesha imani ya Wakenya katika utendakazi wa tume hiyo endapo bunge litaidhinisha uteuzi wake.

Ijumaa, Bw Mbarak aliwaacha wabunge vinywa wazi alipofichua kuwa amewahi kupokea mafunzo katika Mashiriki ya Ujasusi Nchini Amerika, FBI na CIA, na kupata ujuzi ambao umemwezesha kuimarisha utendakazi wake katika asasi zote ambazo amewahi kuhudumia.

Pia, alielezea kwa kina tajriba yake kama afisa wa jeshi, afisa wa ujasusi katika jeshi, Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS), iliyokuwa Tume ya Kupambana na Ufisadi Nchini (KACC) na wadhifa wake wa sasa katika KenGen.

Aliwaambia wabunge kwamba, atachapa kazi kwa mujibu wa sheria na bila mapendeleo na kuahidi kujiuzulu ikiwa mtu yeyote atadhubutu kushawishi kazi yake kwa njia yoyote, haswa kisiasa.

Bw Mbarak, ambaye ni afisa wa usalama na maadili katika kampuni ya uzalishaji umeme, KenGen, jana aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kwamba, atapambana na ufisadi katika serikali kuu na zile za kaunti kwa kuwalenga washukiwa wote bila kujali nyadhifa zao.

“Dhana kwamba kuna watu au afisi fulani yenye ushawishi ambayo huingilia utendakazi wa EACC haitakuwepo chini ya uongozi wangu. Na endapo kutatokea ushawishi kutoka afisi yoyote ambao utaingilia utendakazi wangu kwa njia moja ama nyingine, nitaamua kujiondoa na kwenda nyumbani kwangu Kilifi,” akasema alipopigwa msasa na kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo.

“Sitakubali amri kutoka popote… Nitawahudumia Wakenya wote kwa usawa,” Bw Mbarak akaeleza.

Afisa huyo wa zamani wa ujasusi katika jeshi la Kenya alisema atachunguza upya faili za kesi zinazowahusu washukiwa wanaoshikilia vyeo vya juu, ambazo zimekwama katika EACC kwa muda mrefu kuhakikisha zinashughulikiwa kwa haraka.

“Najua kuna faili ambazo zimedumu katika tume hii kwa zaidi ya miaka saba. Hizi ndizo nitashughulikia kwa haraka endapo kamati hii itaidhinisha uteuzi wangu,” Bw Mbarak akasema.

“Na nitahakisha hilo kwa kutekeleza mabadiliko katika afisi kuu. Nitahakikisha kila afisa anafanya kazi aliyohitimu kufanya… na hili litawezakana tu kupitia upigaji msasa upya,” Bw Mbarak alieleza.

Aliwaomba wabunge kuzifanyia marekebisho sheria za EACC haswa sheria inayohusu kutwaliwa kwa mali zote zilizopatikana kwa njia ya ufisadi.

“Kwa sababu nitakuwa nikiwajibikia bunge katika utendakazi wangu, naomba kamati hii kuhakikisha kuwa EACC imepewa meno kisheria kuweza kutwa mali ya washukiwa wote wa ufisadi. Kwa sasa kuna udhaifu fulani wa kisheria ambao unahujumu uwezo wa tume hii kutwaa mali ya wezi wa rasilimali za kitaifa,” akasema.

Bw Mbarak aliwasisimua wabunge alipoelezea tajriba yake kama afisa wa jeshi, afisa wa ujasusi katika jeshi, Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS), iliyokuwa Tume ya Kupambana na Ufisad Nchini (KACC) na wadhifa wake wa sasa katika KenGen.

Bw Mbarak alisema ufanisi huu ulichangiwa pakubwa na mamake mzazi ambaye alijinyima anasa za dunia ili kufadhili masomo yake.

Alipandwa na hisia na kudondokwa machozi alipokuwa akielezea mchango wa mamake maishani mwake.