MakalaSiasa

UFISADI: Kaunti yanunua ng'ombe kwa Sh3.7 milioni!

March 27th, 2019 3 min read

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI ya Kaunti ya Kisumu ilitumia Sh3.7 milioni kununua ng’ombe mmoja wa maziwa, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Edward Ouko inaonyesha.

Ripoti hiyo ya mwaka wa fedha wa 2017/2018, inaeleza kuwa pesa hizo zililipwa kwa mfanyabiashara mmoja, ambaye kulingana na rekodi alipasa kuuzia kaunti hiyo ng’ombe 27 wa maziwa aina ya “Ayrshire”, lakini uchunguzi ukabainisha ni ng’ombe mmoja pekee aliyewasilishwa.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, mbali na Kisumu, kaunti nyingi zilitumia mamilioni ya pesa kulipia bidhaa na huduma ambazo hazikutolewa.

Kaunti hizo ziliripoti kutumia fedha kwa ununuzi wa bidhaa na huduma tofauti, lakini Mkaguzi Mkuu alipochunguza ilipatikana hapakuwa na huduma ama bidhaa zilizotolewa.

Kwa jumla, Bw Ouko ametilia doa karibu kila kaunti kwa masuala kama vile kuajiri idadi kubwa ya wafanyakazi kupita kiasi, kutotumia mfumo bora wa kuthibitisha uhalali wa matumizi ya fedha, kutokuwepo usawa wa kijamii katika ajira na kutokamilishwa kwa miradi ya maendeleo.

KISUMU

Ripoti hiyo inasema kuwa hapakuwa na stakabadhi zozote za kuthibitisha kaunti hiyo inayoongozwa na Prof Anyang’ Nyong’o ilipokea ng’ombe wengine 26 kama ilivyodai.

Ripoti hiyo imetilia shaka pia Sh9.8 milioni, ambazo zilidaiwa kulipwa kwa kampuni tofauti kuuzia kaunti hiyo mbegu na mbolea. Pia kampuni hizo zilionekana kumilikiwa na mtu mmoja.

NAIROBI

Mpango wa kurembesha jiji la Nairobi ulimeza Sh18.8 milioni kwa malipo ya vibarua pekee, ingawa hapakuwa na stakabadhi zozote za kuthibitisha uhalali wa malipo haya.

Afisi Gavana Mike Sonko na naibu wake (ambaye hajakuwepo kwa zaidi ya mwaka mmoja) ilitumia Sh14.4 milioni na kusema maelezo kuhusu matumizi hayo ni siri, kwa sababu fedha hizo zilitumiwa kwa masuala ya kiusalama.

“Sheria inaruhusu serikali kuu pekee kutumia fedha kwa masuala ya kisiri. Kwa hivyo serikali ya kaunti ilikiuka sheria,” akasema Bw Ouko.

MOMBASA

Kaunti ya Mombasa haijawasilisha Sh3.5 bilioni kwa mashirika mbalimbali zinazokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi kugharamia malipo kama vile ushuru kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), malipo ya uzeeni (NSSF) na ada za Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF).

GARISSA

Kaunti ya Garissa ilimlipa mwanakandarasi Sh3.9 milioni kurembesha mji lakini hakutekeleza majukumu yake. Kaunti hii ilidai pia kutumia Sh6.6 milioni kulipia huduma za hotelini ambazo hazingeweza kuthibitishwa.

EMBU

Kaunti ya Embu ina Sh358,563,651 kwenye akaunti 32 katika benki tofauti za humu nchini. Bw Ouko alisema akaunti hizi zilifunguliwa kinyume na sheria za usimamizi wa fedha za umma katika kaunti na hivyo basi afisi ya gavana ilikiuka sheria.

BARINGO

Serikali ya Kaunti ya Baringo ilinunua dawa za matibabu kwa Sh13.5 milioni ilhali kulikuwa na muuzaji ambaye aliwasilisha ombi kuuzia kaunti dawa hizo kwa Sh6.8 milioni pekee.

MERU

Mfanyabiashara alilipwa jumla ya Sh1.8 milioni kuuzia Kaunti ya Meru mapipa 600 ya plastiki yenye ukubwa wa lita 2,000 kila moja. Mhasibu Mkuu alitilia shaka utumizi huu wa fedha kwani kulingana naye, mapipa hayo yalistahili kugharimu Sh1,000 kila moja na wala si Sh3,000 kila moja. Kwa msingi huu, serikali ya kaunti ingetumia Sh600,000 pekee kwa jumla.

KIAMBU

Kaunti ya Kiambu ilimumunya karibu Sh10 milioni kwa ununuzi wa miche ya parachichi bila kufuata kanuni za kisheria.

Ripoti inasema kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Ferdinand Waititu ilitumia Sh9.97 milioni kununua miche hiyo aina ya ‘Hass’ kwa njia isiyoeleweka.

“Zabuni ya kununua miche hiyo ilipeanwa kwa kampuni mbili pekee. Hapakuwa na maelezo ya kuridhisha kuhusu kwa nini hatua hii isiyo ya kawaida ilichukuliwa,” akasema Bw Ouko kwenye ripoti yake.

NYERI

Serikali ya Kaunti ya Nyeri imekosolewa ilipopatikana na dawa zilizogharimu Sh15.2 milioni ambazo zilikuwa zimeharibika katika hospitali 31.

“Hapakuwa na maelezo kuhusu kwa nini dawa zilikuwa zimenunuliwa kwa wingi kupita kiasi, hali iliyosababisha ziharibike na hivyo kuharibu pesa za umma,” ripoti ikaeleza.

KITUI

Mpango wa kuwezesha wakazi kupanda pojo almaarufu kama ‘Ndengu Revolution’ uliogharimu Sh49.6 umetiliwa shaka.

Afisi ya Gavana Charity Ngilu ilikuwa imesema fedha hizo zilitumiwa kununua mbegu, lakini Mhasibu Mkuu kwenye ripoti yake anaeleza haiwezekani kutambua kama mpango huo umenufaisha wakazi.

Wakati huo huo, mbegu nyingine zilikuwa zikipeanwa na shirika la Kenya Red Cross kwa wakulima na hivyo basi ikawa vigumu kutambua kiwango halisi ambacho kilitoka kwa serikali ya kaunti.