HabariSiasa

UFISADI: Mawaziri watano wamulikwa

February 21st, 2019 2 min read

WYCLIFFE MUIA Na RUTH MBULA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alijitenga na mawaziri wafisadi akisema watakaopatikana na makosa wabebe misalaba yao kwa kufungwa gerezani na mali yao kutwaliwa.

Akihutubu Jumatano akiwa ziarani Kaunti ya Kisii, Rais alisema: “Wezi wa mali ya umma hawapaswi kuhusisha jamii zao katika maovu yao. Kila mtu abebe msalaba wake.”

Hii ni kuhusiana na uchunguzi unaoendelea ukilenga takriban mawaziri watano kuhusiana na madai ya kula hongo kutoka kwa kampuni zinazopewa tenda katika wizara zao.

Duru zinadokeza kuwa Rais Kenyatta amechukua muda kuwafuta mawaziri hao, akisubiri ripoti ya uchunguzi unaoendeshwa na Idara ya Upelelezi (DCI) chini ya George Kinoti na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inayoongozwa na Twalib Mbarak.

Maafisa wa wa EACC waliambia Taifa Leo kuwa uchunguzi huo pia unahusisha magavana kadhaa wa sasa na wa zamani.

Waziri wa Utalii, Najib Balala tayari amepokea mwaliko wa kukutana na maafisa wa EACC kuhusiana na madai ya ufisadi katika wizara yake.

Mwenzake wa Fedha, Henry Rotich alihojiwa mnamo Jumatatu katika afisi ya DCI kuhusiana na kashfa ya ujenzi wa mabwawa mawili yaliyogharimu Sh65 bilioni. Ujenzi wa mabwawa hayo, Arror na Kamwarer, katika eneo la Keiyo Kusini, Kaunti ya Elgeyo Marakwet umekwama licha ya serikali kuwekeza mabilioni ya pesa.

EACC Italia

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa tayari maafisa wa EACC na wale wa DCI wamekita kambi nchini Italia kuchunguza utoaji kandarasi wa ujenzi wa mabwawa hayo, ambao unashukiwa kukumbwa na utoaji hongo.

Kampuni ya CMC di Ravenna, yenye makao yake makuu nchini Italia, imepewa kandarasi ya kujenga bwala la Arror kwa Sh38.5 bilioni na la Kimwarer kwa Sh28 bilioni.

Jumatatu iliyopita, EACC ilikuwa imemwandikia Waziri Balala ikimtaka kufika mbele yake kuhusiana na sakata ya Sh100 milioni zilizolipwa na wizara yake kwa kampuni ya American Society of Travel Agents (ASTA), kutangaza utalii wa Kenya mnamo 2017.

Tayari aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Utalii, Fatuma Hirsi pamoja na maafisa wengine wakuu wa wizara hiyo wamefika mbele ya EACC kuhusiana na kashfa hiyo.

Mawasiliano ya ufisadi

EACC ilidokezea Taifa Leo kuwa Waziri Balala amehusishwa na kashfa hiyo baada ya stakabadhi kuonyesha kuwa alikuwa anawasiliana kila mara na maafisa wa ASTA walioko Kenya.

Naye Waziri wa Elimu, Amina Mohammed anatarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu, kuelezea madai ya ufisadi katika usambazaji wa vitabu katika shule za umma nchini.

Bi Amina anatarajiwa kutoa maelezo kuhusu usambazaji wa vitabu vingi kupita kiasi katika shule za umma, hatua ambayo inashukiwa kunufaisha baadhi ya maafisa katika wizara yake na wachapishaji.

Maafisa wa EACC na wale wa DCI pia wanalenga magavana kadhaa kuhusiana na wizi wa mali ya umma.

Jumatano, maafisa wa EACC walikagua afisi na makazi ya Gavana wa Samburu, Moses Kasaine mtaani Karen, Nairobi wakitafuta stakabadhi kuhusiana na wizi wa Sh2 bilioni za kaunti.