Makala

Ufisadi Murang’a madaktari wakidai malipo ya huduma yatumwe kwa simu zao binafsi

May 4th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MNAMO Mei 1, 2024, Taifa Leo ikiwa na fununu kwamba katika hospitali kuu ya Murang’a kulikuwa na ufisadi uliokolea kitengo cha matibabu ya meno, tuliandamana na mama mmoja aliyekuwa akisaka huduma za mtoto wake kung’olewa jino.

Ingawa madaktari wamesemwa kuwa katika mgomo, Taifa Leo ilibaini kwamba kuna wale ambao wanaendelea kuhudumia wagonjwa katika hospitali hiyo, lakini baadhi yao wakijipa vya haramu kupitia ufisadi.

Kwa kuwa serikali ya kaunti imeweka kamera za siri (CCTV) katika hospitali hiyo na kuhitaji kwamba kila mgonjwa ajisajili kielektroniki, mama huyo akiandamana na mtoto wake msichana aliwasili katika hospitali hiyo mwendo wa saa tatu asubuhi.

Mwandishi wa Taifa Leo aliwasindikiza na kujitambulisha tu “niko nao”.

Mgonjwa alipokelewa kwa kuhitajika kutoa habari zake kamili ndipo ziwekwe katika faili kwa kompyuta. Taarifa hizo zilipeanwa na mama mzazi.

Licha ya kuwa huduma hiyo ya usajili haina malipo yoyote, mama mtoto aliambiwa kwamba alihitajika kuilipia Sh200.

Ajabu ni kwamba, mikakati ile alipewa ya kulipa gharama hiyo ya Sh200 ni ile ya malipo ya huduma za kimatibabu kama ilivyotolewa katika mwongozo wa serikali ya kaunti na ambapo kung’olewa jino moja ni Sh200.

Hii ina maana kwamba, gharama hiyo ya Sh200 haikuwa ya usajili kama mgonjwa bali ilikuwa malipo ya kung’olewa jino.

Baada ya kujisajili, mama aliingia na mtoto wake wa umri wa miaka 12 hadi kwa ‘daktari wa meno’ na ambapo aliagizwa sasa alipe Sh200 za huduma hiyo.

Baada ya mama mtoto kuteta kwamba alikuwa amelipa ada hiyo, aliambiwa kwamba tangu mgomo uanze, serikali imezindua mbinu mpya ya kukusanya ushuru wa kuwalipa pesa wanazodai na ndipo ada za usajili wa wagonjwa zikawekwa.

Lakini kilichomshangaza zaidi ni wakati mtaalamu huyo wa meno alimwelekeza mama mtoto kutuma pesa hizo kwa nambari ya simu ya kibinafsi, daktari huyo akiongeza kwamba “mitambo ya kupokezwa malipo hayo ina hitilafu kufuatia kupotea kwa huduma za intaneti”.

Baada ya mama mtoto kuteta kwamba alikuwa amelipa pesa za awali kupitia mtambo huo maalum wa kaunti na haukuwa na shida, alielekezwa kwamba aende nyumbani na arejee siku iliyofuata “kwa kuwa hata tumegoma”.

Ndipo mama mtoto alifanya uamuzi wake wa kurejea nyumbani na mtoto wake jino likiwa bado linamuuma au atii wito huo wa kutuma pesa kwa nambari ya kibinafsi ya simu.

“Mimi nitatuma tu kwa kuwa sina namna nyingine. Lakini nitahifadhi ujumbe huo wa simu ulio na jina la aliyepokea pesa hizo na hatimaye nilalamike kwa serikali ya kaunti kuhusu ufisadi huo wa wazi,” akasema kwa Taifa Leo.

Aling’ang’ana na kulipa gharama hiyo ya shaka.

Ni baada ya kutii agizo hilo linalodhaniwa kuwa la ufisadi ambapo mtoto alihudumiwa na jino lake lililokuwa na shida likang’olewa.

Mnamo Mei 3, 2024, mama huyo alituma ujumbe huo wa malipo kwa afisa mmoja wa serikali ya kaunti na kuelezea kuhusu masaibu aliyoyapitia hadi awamu hiyo anayoshuku kuwa ya ufisadi.

Hata hivyo, hadi wakati wa kuchapisha habari hii, afisa huyo ambaye yuko kiwango cha waziri wa kaunti, hakuwa amejibu ujumbe huo.