Habari

Ufisadi: Muturi alaumu EACC, DCI

July 18th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amezielekezea lawama asasi za kupambana na ufisadi akisema ndizo zimefeli kufanikisha vita dhidi ya uovu huo nchini.

Amesema bunge limekuwa likitoa mapendekezo yake baada ya kuendesha uchunguzi kuhusu sakata mbalimbali za ufisadi lakini asasi husika zimefeli katika wajibu wao wa kuhakikisha watuhumiwa wanaadhibiwa.

“Sisi kama asasi ya bunge tumekuwa tukichunguza kashfa mbalimbali za ufisadi na kuwalisha ripoti kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI). Lakini inasikitisha kuwa asasi hizo zimeshindwa kuchukua hatua kuhakikisha kuwa washukiwa wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” Bw Muturi amesema Alhamisi.

Bw Muturi amesema hayo alipoongoza hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Kimkakati wa Muungano wa Wabunge wa Afrika Dhidi ya Ufisadi (APNAC), tawi la Kenya, katika Intercontinental Hotel, Nairobi.

Maafisa kuhudhuria vikao

Amesema huenda bunge likalazimishwa kufanya marekebisho ya sheria zake kutoa nafasi kwa maafisa wa EACC na DCI kuhudhuria vikao vya kamati zake vya kuchunguza sakata za ufisadi.

“Kwa namna hii maafisa hao wataweza kukusanya ushahidi wote wanaohitaji kuwawezesha kuwafunguliwa mashtaka washukiwa wa ufisadi. Mtindo kama huu unafuatwa katika taifa jirani la Uganda ambako umebainika kuzaa matunda,” amesema Bw Muturi.

Hata hivyo, amewahimiza Wakenya kutovunjika moyo na kuendelea kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi ambao aliutaja kama “kansa” hatari ambayo inaweza kuangamiza nchi hii ikiwa haitadhibitiwa.

Kwa upande wake, kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ambaye alihudhuria shughuli hiyo aliitaka Serikali kuongeza mgao wa fedha kwa asasi za kupambana na ufisadi.

“Ni kinaya kwa serikali kukariri imejitolea kuangamiza ufisadi ilhali fedha ambazo asasi kama EACC na DCI hutengewa kufadhili mchakato huo ni finyu zaidi. Mbona serikali itenge chini ya Sh10 bilioni kwa asasi hizi ilhali zinapaswa kufuatiliwa wizi wa zaidi ya Sh600 bilioni kwa mwaka?” akauliza Bw Mudavadi.