HabariSiasa

Ufisadi ni hatari kuliko Ebola – Wabukala

June 18th, 2019 1 min read

Na BENSON AMADALA

MWENYEKITI wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Askofu Mkuu (mstaafu) Eliud Wabukala amewataka Wakenya kukoma kuwasifu viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakihusishwa na kashfa za ufisadi.

Alisema ufisadi umeathiri uchumi wa nchi hivyo unafaa kukabiliwa vilivyo.

Alisema watu waliohusishwa na sakata mbalimbali za ufisadi hawafai kupewa nyadhifa za umma hadi pale watakapojitakasa.

“Ufisadi ni mbaya kuliko Ebola. Tukikabili ufisadi sawa na tunavyopigana na Ebola itachukua siku moja pekee kuwatia mbaroni na kuwafikisha mahakamani watu wafisafi,” akasema Bw Wabukala.

Bw Wabukhala, aliyekuwa akizungumza katika Kaunti ya Kakamega, alisema ufisadi umekolea katika kila sekta serikalini kwa sababu baadhi ya watu walio uongozini wamekuwa wakiwalinda wahusika.

“Tume ya EACC imeanzisha juhudi za kukabiliana na watu wanaoshikilia nyadhifa katika afisi za umma kama njia mojawapo ya kuangamiza zimwi la ufisadi,” akasema Bw Wabukala.

Mwenyekiti huyo wa EACC alikuwa akihutubia warsha ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Miradi ya Maji katika Ukanda wa Ziwa Victoria.

Aliwataka Wakenya kujitolea kukabiliana na ufisadi kuanzia kiwango cha familia hadi ngazi ya kitaifa.

Tume ya EACC imekuwa ikilaumiwa kwa kukosa kutumia mamlaka iliyopewa kuwakabili washukiwa wa wizi wa pesa za umma.