Makala

UFISADI: Nini muhimu kati ya urafiki na taifa?

February 27th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wa matabaka mbalimbali wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwasimamisha ama kuwafuta kazi mawaziri ambao wametajwa kwenye kashfa za ufisadi.

Wadadisi wa masuala ya utawala na siasa pamoja na wananchi waliohojiwa na Taifa Leo walisema mawaziri hao wanafaa kuwa nje ya nyadhifa zao uchunguzi unapoendelea, ili kulinda wasitatize shughuli hiyo, na wale watakaopatikana kuhusika washtakiwe mahakamani, na wasio na makosa warudishwe kazini.

Wadadisi wanasema kushindwa kuwafuta kazi mawaziri hao ni sawa na kuendeleza vita dhidi ya ufisadi kwa ubaguzi, jambo ambalo litatatiza vita dhidi ya ufisadi.

Ingawa Rais Kenyatta amewaonya mawaziri wanaochunguzwa kwamba watabeba msalaba wao, hajawachukulia hatua licha ya wizara wanazosimamia kumulikwa kwa kupoteza mabilioni ya pesa za umma.

Wadadisi wanasema kujivuta kwa Rais kuwachukulia hatua kunatokana na uhusiano wake wa kirafiki na kisiasa na mawaziri hao, suala ambalo linamuacha kwenye njia panda.

“Nafikiri Rais anafaa kutenganisha urafiki, uwe wa kisiasa, kijamii au kibiashara na uongozi wa nchi ikiwa anataka kushinda vita dhidi ya ufisadi,” alisema mdadisi wa masuala ya utawala, Bw David Singano.

Alieleza kuwa, japo Rais ameonyesha nia ya kukabiliana na rushwa, anafaa kudhihirisha kujitolea kwake kwa kuwasimamisha kazi mawaziri wake wanaoshukiwa kushiriki ufisadi, ama wizara zimepoteza fedha chini ya usimamizi wao.

“Ikiwa anajivuta kuwachukulia hatua mawaziri wake kwa sababu moja au nyingine, basi hatakuwa akifanyia Wakenya haki. Hafai kuwaambia wajiuzulu, anafaa kuwapiga kalamu,” akaeleza Bw Singano.

“Alifanya hivyo 2015 wakati alipowaagiza Charity Ngilu, Michael Kamau, Kazungu Kambi, Felix Koskei na Davies Chirchir kujiuzulu. Hakuna kinachomfunga Rais kufuta ama kuvunja baraza lake la mawaziri wakati wowote bila kushauriana na yeyote,” asema Bw Singano.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Bw Barrack Muluka, kujivuta kwa rais kuwatimua mawaziri wanaohusishwa na ufisadi kunatokana na muundo wa baraza la mawaziri.

Hata hivyo, anasema jukumu la kuunda baraza la mawaziri ni la rais na anafaa kuwachukulia hatua asiporidhishwa na utendakazi wao.

Kuna mawaziri sita ambao wizara zao zinachunguzwa na Mamlaka ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), pamoja na Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI), kuhusu kashfa za mabilioni ya pesa, ambapo baadhi ya maafisa walio chini ya mawaziri hao wameshtakiwa.

Katika Wizara ya Kilimo, ambayo inasimamiwa na mwandani wa Rais, Mwangi Kiunjuri, Katibu wa Wizara, Richard Lesiyampe na maafisa walio chini yake wanakabiliwa na kesi kuhusu kashfa katika wizara hiyo.

Licha ya kumuonya Bw Kiunjuri hadharani mara kadhaa, Rais Kenyatta hajamchukulia hatua huku wakulima nchini wakiendelea kuteseka.

Katika sakata ya pili ya Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), ambapo yadaiwa Sh8 bilioni ziliporwa, ni katibu wa wizara Lilian Omollo na maafisa wengine ambao wamebeba msalaba.

Bi Sicily Kariuki, ambaye alikuwa Waziri katika Wizara ya Ugatuzi wakati pesa zinadaiwa kuporwa, hajachukuliwa hatua na sasa ni Waziri wa Afya.

Wadadisi pia wanashangaa ni kwa nwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwini Rais amechelewa kuwaangushia shoka mawaziri ambao uchunguzi wa DCI unaeleza kuwa wamekuwa wakipokea hongo kutoka kwa wanakandarasi wanaopatiwa tenda za serikali.

Uchunguzi wa DCI na EACC umeonyesha kuwa baadhi ya mawaziri walisafiri ng’ambo kupokea hongo kutoka kwa kampuni za kimataifa.

Miongoni mwa mawaziri ambao wamehojiwa na wapelelezi kuhusu madai hayo ni Waziri wa Fedha, Henry Rotich na mwenzake wa Utalii, Najib Balala.

Rais Kenyatta na Bw Rotich wamekuwa marafiki kwa miaka mingi, tangu Rais alisimamia Wizara ya Fedha kwenye utawala wa Rais Mstaafu, Mzee Mwai Kibaki.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i, Rotich na Bw Kiunjuri pia wametajwa kwenye ripoti ya kamati ya bunge kuhusu sakata ya mahindi. Mawaziri hao walikuwa wanachama wa kamati ya mawaziri kuhusu chakula wakati sakata ya mahindi ilipozuka.

Rais Kenyatta anamwamini sana Bw Bw Matiang’i, ambaye amedhihirisha kuwa mchapa kazi, na amemuongezea majukumu kwa kumteua kusimamia kamati ya kushirikisha miradi ya serikali katika wizara zote.

Nayo Wizara ya Maji inayosimamiwa na Simon Chelugui, inachunguzwa baada ya kubainika kuwa huenda serikali ilipoteza mabilioni ya pesa kupitia ujenzi wa mabwawa hewa katika kaunti za Elgeyo Marakwet na Nakuru.