HabariSiasa

UFISADI: Raila awakosoa wandani wa Ruto

December 11th, 2018 2 min read

ONYANGO K’ONYANGO na ERIC WAINAINA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amepuuzilia mbali wanasiasa wanaodai kwamba vita vya ufisadi vimeingizwa ukabila.

Kwa muda sasa, baadhi ya viongozi kutoka eneo la Rift Valley ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto, wamekuwa wakidai vita hivyo dhidi ya ufisadi vinalenga jamii ya Wakalenjin kwa nia ya kumharibia nafasi Bw Ruto kushinda urais ifikapo mwaka wa 2022.

Lakini akiongea akiwa katika Kaunti ya Kiambu, Bw Odinga alisema hakuna mtu anayeiba pesa kwa niaba ya jamii anayotoka na wanaoiba mali ya umma wanafaa kubeba msalaba wao kibinafsi.

Huku Bw Odinga akisema hayo, mgawanyiko uliibuka kati ya wanasiasa wa jamii ya Wakalenjin kuhusu vita dhidi ya ufisadi huku kundi moja likidai kuwa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wanalenga kummaliza kisiasa Bw Ruto kwa kuhusisha watu kutoka jamii hiyo na uovu huo.

Hata hivyo, kundi jingine linasema kuwa wale wanaohusika katika ufisadi wakome kuhusisha jamii nzima. Makundi hayo mawili yameibuka siku chache baada ya Bw Ruto kutaka taasisi zinazopigana na ufisadi kutekeleza majukumu yao bila ubaguzi na kuepuka kutumiwa kusuluhisha tofauti za kisiasa.

Mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono alidai Rais Kenyatta na Bw Odinga wana njama ya kuwakamata washirika wa Bw Ruto wanaoshikilia nyadhifa za juu serikalini wakilenga kummaliza kisiasa.

“Vita hivi ni vya kisiasa na Rais anatumia muafaka wake na Bw Odinga kujaribu kummaliza Bw Ruto. Wawili hao wanamkata miguu Naibu Rais kwa sababu zinazojulikana,” alisema Rono akiongea kwa simu na kusema kwamba azma ya Bw Ruto ya kuingia Ikulu 2022 haiwezi kuzimwa na yeyote.

Wakiongea wakiwa mjini Eldoret, Seneta wa Nandi Samson Cherargei na Mbunge wa Aldai Cornelius Serem, walidai kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga wataalamu kutoka jamii ya Wakalenjin ili kuvuruga dhamira ya Bw Ruto kuwa Rais mwaka wa 2022.

“Tunaunga vita dhidi ya ufisadi lakini kama viongozi kutoka Rift Valley, tunasimama na wataalamu wetu kwa sababu vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi vinatumiwa na watu wachache kusuluhisha tofauti za kisiasa,” alidai Bw Cherargei.

Bw Serem alidai kwamba vita dhidi ya ufisadi vinalenga wakuu wa mashirika ya serikali wanaotoka katika jamii ya Wakalenjin akisema kuna mashirika zaidi ya 300 na baadhi yayo yanasimamiwa na watu fisadi ambao hawajakamatwa.

Hata hivyo, madai yao yalipuuzwa na kundi jingine la wabunge wanaosema, watu wanaopora mali ya umma wanafaa kuchukuliwa hatua za kisheria kama watu binafsi na sio jamii. Mbunge wa Cherang’any Joshua Kutuny na mwenzake wa Nandi Hills Alfred Keter waliwataka wenzao kukoma kutoa taarifa za kupotosha na kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi akisema ufisadi utaua uchumi iwapo hautaangamizwa.

Bw Kutuny na Bw Keter walisema kwamba vita hivyo havifai kuhusishwa na siasa za urithi za 2022.

Alisema madai kwamba vinalenga kuhujumu azma ya Bw Ruto kuwa Rais ni ya kupotosha.