HabariSiasa

UFISADI: Ruto akosa msimamo

March 3rd, 2019 3 min read

Na WAANDISHI WETU

Naibu Rais William Ruto amedhihirisha kuwa mwanasaisa asiyekubali kupitwa na mjadala wowote lakini pia anayegeuza msimamo wake haraka hasa katika kutetea maslahi yake ya kisiasa na kibinafsi.

Hii ni hulka ambayo amekuwa akiendeleza lakini kutokana na ustadi wake wa kuzungumza watu wengi hukosa kung’amua anapobadilisha msimamo.

Dkt Ruto huwa mwepesi wa kubadilisha msimamo katika masuala ambayo ama yanamgusa moja kwa moja au wandani wake wa karibu.

Japo amekuwa akisisitiza kwamba vita dhidi ya ufisadi havifai kuingizwa siasa, wakosoaji wake wanashangazwa na hatua yake ya kuingilia mradi wa ujenzi wa mabwawa mawili katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Akiongea katika majengo ya Mahakama ya Juu mnamo Alhamisi Dkt Ruto alitaja kama “uongo mtupu” madai ya Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti, kuwa Sh21 bilioni zimepotea katika mpango wa ujenzi wa mabwawa hayo yanayotarajiwa kugharimu Sh63 bilioni.

Bw Ruto mwenyewe amekuwa akitaka wanasiasa kuachia asasi huru uchunguzi wa sakata za ufisadi tofauti na anavyofanya sasa. Baadhi ya wabunge wamemsuta huku wakisema kauli yake ni sawa na kuingilia uchunguzi na kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi, hasa baada ya wandani wake kushukiwa kuhusika.

Kuanzia kwa mzozo wa umiliki wa hoteli ya Weston, kunyakuliwa kwa shamba la mkimbizi wa ndani kwa ndani, Bw Adrian Muteshi hadi sakata ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), kauli za Ruto katika masuala hayo zimekuwa za kupinga uhalisia wa mambo. Lakini baada ya muda, kauli zake hubainika kuwa sio za kweli naye akawa analazimika kugeuza msimamo.

Mnamo 2009, Bw Muteshi alipodai kuwa Dkt Ruto alinyakua shamba lake la ukubwa wa ekari 100, mbunge huyo wa zamani wa Eldoret Kaskazini alikana. Badala yake alidai kuwa aliuziwa shamba hilo na Bi Dorothy Yator, lakini baadaye alibadili kauli baada ya Muteshi kuwasilisha kesi kortini na kukubali kumrejeshea shamba hilo.

Hali kama hiyo iliibuka kuhusu uhalali wa ununuzi wa ardhi kulikojengwa hoteli ya Weston ambapo Dkt Ruto alikana madai kuwa ilinyakuliwa kutoka kwa mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege (KCAA)

Awali, Ruto alipinga madai kuwa yeye ni mmiliki wa hoteli hiyo, akisema mali hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Bw Patrick Osero.

Lakini mwezi jana akiongea jijini London, Uingereza, Naibu Rais alikubali kuwa yeye ndiye mmiliki wa hoteli hiyo na kwamba wale waliomuuzia ardhi hiyo ndio wanaofaa kuchukuliwa hatua kwa kosa la unyakuzi wa ardhi.

Tangu idara za Uchunguzi za DCI, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) zilipoanza kuwinda wezi wa mali ya umma na maafisa kadhaa wa ngazi za juu kuhojiwa ama kushtakiwa, Dkt Ruto mara kadhaa amejipata akijibizana na viongozi wa upinzani kuhusu vita hivyo.

Wakati wa kongamano kuhusu ufisadi lililoandaliwa Januari 25 mwaka huu, Naibu Rais alisifu juhudi zilizopo za kumaliza ufisadi nchini.

“Hili ni kongamano muhimu sana. Rais ulipoanzisha juhudi za kujenga idara za kupigana na ufisadi nchini, ulipotenga pesa, rasilimali na watu kumaliza ufisadi, wengi hawakuamini kuna kitu tofauti ambacho kingefanyika.

Lakini leo, Wakenya wamekubali kuwa kusudio lako lilikuwa zuri,” Dkt Ruto alisema alipokuwa akihutubu katika kongamano hilo. Akipinga kauli kuwa upinzani ndio uliokuwa unachangia pakubwa katika vita dhidi ya ufisadi, Naibu Rais alisema, “Msiweke siasa katika vita dhidi ya ufisadi, tuachie idara huru kufanya kazi hiyo, tuna wanaume na wanawake waliohitimu ambao wanafanya kazi hiyo, tuna Idara ya Mahakama inayoweza kutatua kesi hizo na Kenya itasonga mbele,” Dkt Ruto akasema mnamo Oktoba 1, 2018.

Hata hivyo, licha ya kusifu idara hizo mara kadhaa, Naibu Rais anazikosoa akidai kuwa mara nyingine vita dhidi ya ufisadi huwa vinalenga watu wa jamii fulani.

“Idara hizo sharti zifanye kazi bila kuingiliwa, bila kupokea maelekezo kutoka kwa yeyote, bila kuangalia jamii, eneo ama upande wowote anaotoka mtu,” Dkt Ruto alisema mnamo Desemba 7.

Matamshi hayo ya kiongozi huyo yalikuja wakati viongozi wa mashirika tofauti ya serikali, ambao, ilibainika wengi walikuwa wa jamii ya Bonde la Ufa, walikuwa wamevamiwa na kukamatwa.

Wakati wa mjadala wa kurekebisha katiba ulipoanza, Bw Ruto aliupinga vikali kabla ya kubadilisha nia na kuunga. Hata hivyo, baada ya muda aliupinga tena.

Huku baadhi ya wakereketwa wa mabadiliko ya katiba wakitaka viti viongozwe serikalini ili jamii nyingi ziwakilishwe,

Naibu Rais amekuwa akitaka kiti cha upinzani pekee kiundwe.