Habari

Ufisadi: Uhuru achemka tena!

March 23rd, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta jana alisisitiza kuwa amejitolea kupigana na ufisadi na kusisitiza kwamba hatawasaza washirika na wandani wake wa kisiasa wanaopora mali ya umma.

“Ikiwa wewe ni fisadi tutakupiga vita. Unaweza kuwa kaka ama dada yangu ama mshirika wangu mkuu wa kisiasa, lakini ikiwa wewe ni fisadi tutakuandama,” alisema Rais Kenyatta.

Hili lilikuwa onyo kali kwa watu ambao wamekuwa wakikwaza vita dhidi ya wizi wa mali ya umma ama kuhusika na ufisadi.

Rais Kenyatta alisema yuko tayari kumkabili yeyote anayejihusisha na ufisadi, bila kujali hadhi yake ama kabila analotoka.

Akihutubia Wakenya wanaoishi Namibia aliko ziarani, Rais alisema kamwe hatakubali yeyote kuwa kisiki katika azma ya kuunganisha taifa na kuapa kuendelea kupigania umoja wa Wakenya.

“Sitazuiwa na ukabila ama hadhi katika azimio langu la kuacha taifa lenye umoja na nitaendelea kupigania umoja wa Kenya,” alisema Rais.

“Ukitafuta nafasi ya uongozi, sharti iwe kwa msingi wa unachotaka kufanya kuhudumia watu wengine, si kujihudumia, iwe ni kazi ya kuwahudumia Wakenya, lakini sio kujihudumia wewe, bibi yako na watoto wako.

“Wapende wasipende, rafiki ama adui, ndugu ama dada, wewe kama unataka kuhusika na mambo ya ufisadi tutapigana na wewe. Unaweza kuwa kaka ama dada yangu, lakini wewe ni adui wa Jamhuri ya Kenya. Hapo lazima tuweke mipaka,” Rais alisema.

Matamshi yake yalijiri wakati kumekuwa na vita vya maneno baina ya kambi tofauti za kisiasa kuhusu vita dhidi ya ufisadi, baadhi wakitetea mamlaka zinazoendesha vita hivyo na wengine wakizikashifu.

Tamko laibua hisia

Tamko la Rais kuwa hajali tena hadhi, urafiki wa kisiasa, uhusiano wa damu ama kabila anapopigana na ufisadi, limeibua hisia kuwa Rais yuko tayari kukabiliana na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakidhani kuwa hadhi zao ni za juu na hawawezi kuguswa.

Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga pamoja na wafuasi wao wamekuwa wakishambuliana kwa maneno kuhusu vita dhidi ya ufisadi.

Katika baadhi ya matukio, wafuasi wa Dkt Ruto wamemlaumu Rais Kenyatta na Bw Odinga wakidai wanatumia vita dhidi ya ufisadi kulenga jamii moja.

“Kama uko na maneno, wacha kutumia serikali, wacha kutumia mkono ambao hauonekani. Jitokeze na useme hautaki William Ruto tena, sisi tutasikia na tutajua ni nini kitafuata,” mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alisema.

Dkt Ruto amekuwa akisisitiza kuwa yeye ndiye Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya na kuwa ana haki ya kufuatilia miradi ya serikali na kukosoa pale anapoona mambo yakienda kombo.

“Vita dhidi ya ufisadi ambavyo havina uadilifu ni ufisadi wenyewe. Ni vita ambavyo vinaendeshwa kwa ubaguzi, kwa kutumia ‘ukweli wa kupikwa’ na kulenga wanasiasa fulani,” akasema Naibu Rais wiki hii alipokuwa akihutubia kongamano la wataalamu.

Vilevile, Dkt Ruto na washirika wake wamekuwa wakitaka Mkurugenzi wa Upelelezi, George Kinoti, kutimuliwa wakidai anatumiwa kisiasa huku naye Rais Kenyatta akisisitiza ana imani naye.

Bw Odinga pamoja na wafuasi wake wamekuwa wakishikilia kuwa vita hivyo vinaendeshwa kwa njia sawa, na kusema kuwa wanaojaribu kuvikwaza ndio wamekuwa wakishiriki ufisadi.

Japo mbeleni Rais amewahi kutoa vitisho kuwa hata nduguye akipatikana na hatia ya ufisadi ataadhibiwa kisheria, matamshi yake ya jana kuwa hata “rafiki wangu wa karibu zaidi kisiasa” ama mtu wa hadhi yoyote ile nchini hatasazwa akipatikana na hatia yamewacha Wakenya na hisia mseto.