Habari

UFISADI: Uhuru ajizolea umaarufu

December 10th, 2018 2 min read

Na WANDERI KAMAU

ZAIDI ya nusu ya Wakenya wanamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kwenye vita vyake dhidi ya ufisadi, umeonyesha utafiti mpya.

Kulingana na utafiti uliotolewa na shirika la Infotrak jijini Nairobi Jumapili, asilimia 52 ya Wakenya wanaunga mkono juhudi zake, huku asilimia 43 wakieleza kutounga mkono juhudi hizo.

Wanaounga mkono walitaja kuridhishwa na kukamatwa kwa maafisa wakuu serikalini, kushtakiwa kwao na ushirikiano mzuri kati ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Hajji na Idara ya Upelelezi (DCI) chini ya George Kinoti.

Wengi walioeleza kutoridhishwa walisema kuwa serikali haijakuwa ikifanya juhudi za kutosha kuwashtaki maafisa wa ngazi za juu, kutochukuliwa hatua kwa wanaopatikana wafisadi na kutohukumiwa kwao. Walisema kuwa lazima wale wanaoshtakiwa wahukumiwe ili kujenga imani yao dhidi ya vita hivyo.

Bunge la Kitaifa na Seneti ziliorodheshwa kama taasisi zilizofanya vibaya zaidi kwenye vita dhidi ya ufisadi.

Bunge lilizoa asilimia 15 pekee ya uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya, huku Seneti ikipata asilimia 16 pekee.

Asasi nyingine ambazo Wakenya walieleza kupoteza imani nazo ni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyozoa asilimia 21, huku Idara ya Polisi ikizoa asilimia 22.

Utafiti huo unajiri huku wabunge wakilaumiwa vikali kwa njama za kutaka kujiongezea marupurupu wakidai wanayopokea kwa sasa “hayatoshi”.

Wabunge wameapa kupiga kura kuupitisha mswada huo, ingawa ungali unajadiliwa.

Mswada huo unapendekeza kuongezwa kwa marupurupu ya usafiri, kuboreshwa kwa bima yao ya afya kati ya masuala mengine.

Hata hivyo, Rais Kenyatta tayari ameapa kwamba hataidhinisha mswada huo, hata ikiwa utawasilishwa kwake.

“Sitautia saini mswada huo, kwani itakuwa sawa na kuwasaliti Wakenya, ambao wanakumbwa na gharama kubwa ya maisha. Mtindo wa viongozi kujiongeza mishahara lazima ukome. Sijali hata ikiwa watanichukia,” akasema Rais wiki iliyopita alipohutubu katika Kaunti ya Kiambu.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga pia amewakosoa wabunge, akiwarai kuwa wajalifu kuhusu changamoto zinazowaathiri Wakenya.

Utafiti ulionyesha kwamba Wakenya wengi wana imani kubwa na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) inayoongozwa na Noordin Haji na Idara ya Upelelezi (DCI) inayoongozwa na George Kinoti.

Asasi hizo zilizoa uungwaji mkono wa asilimia 49 na 41 mtawalia.

Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo la utafiti (Infotrak) Angela Ambitho alitaja hayo kuchangiwa na juhudi za afisi hizo mbili kushirikiana kwenye vita dhidi ya ufisadi.

“Wakenya wengi walielezea kuridhishwa na utendakazi wa pamoja wa taasisi hizo mbili kwenye juhudi za kuwakabili wafisadi,” akasema Bi Ambitho.

Kuhusu miito ya kuandaliwa kwa kura ya maoni kuirekebisha katiba, Wakenya wanaonekana kugawanyika mara mbili. Wale wanaounga mkono ni asilimia 44, huku wale wanaopinga wakiwa asilimia 45.

Vilevile, mwafaka wa kisiasa wa Rais Kenyatta na Bw Odinga unaonekana kupokewa vizuri, kwani asilimai 69 ya Wakenya walieleza kuunga mkono huku asilimia 17 pekee wakieleza kutouunga mkono.

Utafiti huo ulijumuisha watu 1,500 na ulifanywa kati ya Novemba 29 na Desemba 1 mwaka huu.