HabariSiasa

UFISADI: Uhuru azimia marafiki simu

August 27th, 2019 2 min read

ANTHONY KITIMO NA MOHAMED AHMED

RAIS Uhuru Kenyatta amesema hatakuwa akijibu simu za watu wanaotaka aingilie kati kuwasaidia wanaponaswa kwenye mtego wa kupambana na ufisadi.

Akizungumza  jijini Mombasa, Rais alisema wakati wa kumuomba aingilie kuwaokoa wanaojipata wakiandamwa na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na Afisi ya Mashtaka ya Umma (DPP) umepita, na sasa ni kila mmoja abebe msalaba wake mwenyewe.

“Kila mahali ulipo, fungua macho na ufikirie kile ambacho unafanya. Hakuna tena ile mahali mtu alikuwa anapiga simu eti ‘eeh, mambo yamekwenda…ni noma nisaidie. Hizo simu zilizimwa. Sasa ni wewe ujitetee,” akasema Rais Kenyatta.

Rais alijitetea kuwa hahusiki katika kuwaambia Mkurugenzi wa DCI, George Kinoti na mwenzake wa DPP, Noordin Haji kuhusu wanayepasa kuandama, akisema wanafanya kazi yao bila yeye kuingilia.

“Wacheni niwaambie kuna wazee wawili wameamua kufa na kupona kufanya kazi hii ya kuchimbua taabu za ufisadi. Hivyo msiseme ni mimi. Mimi sijatuma mtu…wewe ndiwe umekutwa ukifanya makosa. Na hawa wazee hawachezi na hawacheki,” akasema.

Akihutubu wakati alipoanzisha rasmi usafirishaji wa mafuta kutoka Kenya katika bandari ya Mombasa, Rais alisema jinamizi la ufisadi lazima lishughulikiwe kikamilifu bila ubaguzi ama kujali hadhi ya mtu katika jamii.

Katika muda wa miezi michache iliyopita wakuu serikalini, mashirika na kampuni za kibinafs wamekamatwa na kushtakiwa kwa madai ya ufisadi.

Kati ya walioshtakiwa ni Waziri wa Fedha Henry Rotich, Katibu Kamau Thugge, Gavana Ferdinand Waititu wa Kiambu na mwenzake wa Samburu Moses Lenolkulal.

Wengine ni wafanyibiashara Bi Tabitha Karanja na mumewe pamoja na Bw Humphrey Kariuki wanaodaiwa kukosa kulipa ushuru wa mabilioni ya pesa.

Rais alidokeza jana kuwa kuna uwezekano wa kukamatwa kwa maafisa wa ngazi za juu katika Halmashauri ya Bandari (KPA) kuhusiana na mradi wa kujenga eno la kupakua mafuta katika Bandari ya Mombasa wa Kipevu.

“Mtu yeyote atakapokamatwa achukue msalaba wake mwenyewe. Hata katika bandari hii, tunajua baadhi ya miradi inachunguzwa. Tunajua unagharimu shilingi ngapi, na ni pesa ngapi mliitisha na mumetumia ngapi. Hivyo basi mujitayarishe wakati ukifika,” akasema Rais Kenyatta.

Mradi huo wa gharama ya Sh40 bilioni umekuwa ukichunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) tangu Januari mwaka huu ambapo tayari faili 30 zimetayarishwa dhidi ya washukiwa.

Faili hizo zilipelekwa kwa Bw Haji lakini zikarudishwa kwa wapelelezi wa EACC jijini Mombasa kwa maagizo ya kujaza mapengo katika uchunguzi.

Kulingana na duru za Taifa Leo, kati ya wale wanaochunguzwa ni Meneja Mkurugenzi wa KPA, Daniel Manduku na mtangulizi wake Bi Catherine Mturi-Wairi. Wengine ni wanachama wa kamati ya kutoa tenda.